Bashir arejea nyumbani kutoka Nigeria
Rais wa Sudan Omar al-Bashir,
ameondoka nchini Nigeria baada ya makundi ya kutetea haki za kibinadam
kwenda mahakamani, kushinikiza serikali kumkamata kuhusiana na tuhuma za
uhalifu wa kivita.
Afisa mmoja wa kibalozi, katika ubalozi wa Sudan
nchini Nigeria, amesema rais Bashir, alirejea nyumbani Jumatatu jioni
kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Muungano wa Afrika ambao alikuwa
akihudhuria.Afisa huyo amesema, rais huyo alikuwa na majukumu mengine ambayo yalikuwa yakimsubiri nyumbani na amekanusha madai kuwa aliondoka kwa sababu ya kuongezeka kwa shinikizo za kukamatwa kwake.
Mahakama ya kimataifa ya Jinai ICC, inamtuhumu rais Bashir kwa kuhusika na mauaji ya halaiki katika eneo la Darfur nchini Sudan.
Muungano wa Afrika umetoa wito kwa wanachama wake kutotekeleza agizo la mahakama ya ICC ya kumkamata rais huyo wa Sudan.
Viongozi hao wa AU wanasema mahakama hiyo ya ICC imekuwa ikiwalenga viongozi wa nchi za Kiafrika pekee.
source:bbcswahili
0 comments: