TAARIFA RASMI YA SERIKALI YA ZANZIBAR KUHUSU VIFUNGU VYA SHERIA JUU YA UHALALI WA RAIS KUENDELEA KUWEPO MADARAKANI
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa taarifa rasmi ya Serikali kuhusu vifungu vya sheria juu ya uhalali wa kuendelea kuwepo madarakani Rais wa Zanzibar. |
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imewahakikishia Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla
kwamba Rais aliyepo madarakani hivi sasa ataendelea kushika madaraka ya
Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi mpaka pale
utaratibu wa Kikatiba na Kisheria wa kumpata Rais utakapokamilika.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akitoa Taarifa
ya Serikali akisisitiza Taarifa ya awali ya Serikali iliyotolewa na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuhusiana na
kauli za kupotosha zinazotolewa na baadhi ya Viongozi wa vyama vya
Kisiasa kuhusu uhalali wa kuendelea kuwepo kwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyopo madarakani pamoja na Serikali
yake.
Balozi Seif aliwaomba Wananchi
wazipuuze kauli za upotoshaji zinazotolewa zikiashira zaidi uvunjifu wa
amani na kuwataka waendee kuwa watulivu na kudumisha amani iliyopo
Nchini.
Alisema Kifungu cha 28 Mbili
{a} cha Katiba ambacho kimekuwa kikitumika katika kutoa tafrisi potofu
kwa Wananchi kwamba Rais aliyopo madarakani atamaliza muda wake wa
miaka mitano kuanzia Tarehe ambayo alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo
cha kuwa Rais.
Balozi Seif alieleza kwamba ni
dhahiri kwamba dhamira ya kifungu hicho cha Katiba ilikuwa kuweka bayana
kuwa kama uchaguzi Mkuu utafanyika na msindi wa kiti chja Urais
atatangazwa rasmi na Tumen ys Uchaguzi, hivyo muda wake wa kuendelea Mtu
kuwa Rais ungemalizika kwa kufuatana na masharti ya Kifungu hicho.
Alifafanua kwa kuwa Tume ya
Uchaguzi haikumtangaza mshindi wa kiti cha nafasi ya Urais ni dhahiri
masharti ya kifungu hicho hayataweza kusimama na hivyo masharti ya
Kifungu cha 28 {1} {a} cha Katiba kitakuwa na nguvu za Kikatiba kumpa
uwezo wa Rais aliyopo madarakani kuendelea na madaraka ya Urais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Alisema Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anapatikana kwa mujibu wa masharti ya
Kifungu cha 27 cha Katiba ambacho Rais anachaguliwa kufuatana na Katiba
Hiyo na kwa mujibu wa Sheria yoyote itakayotungwa na Baraza la
Wawakilishi hukusu Uchaguzi wa Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi.
Balozi Seif alifahamisha kuwa
ili Rais wa Zanzibar apatikane kwa mujibu wa Katiba na sheria ya
Uchaguzi nambari 11 ya Mwaka 1984, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inapaswa
kuendesha uchaguzi na hatimae kumtangaza mshindi wa nafasi ya Urais
ambae atashika madaraka hayo pale ambapo atakuwa ameapishwa rasmi kwa
mujibu wa kifungu cha 31 cha Katiba ya Zanzibar.
Alisema Kifungu cha 28 {1} {a}
cha Katiba kinaweka utaratibu kuhusu muda wa kuendelea kuwa kuwa Rais,
na kwamba kwa kufuatana na kifungu hicho, mtu aliyechaguliwa kuwa Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ataendelea na dhamana
hiyo mpaka pale ambapo Rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais.
Alieleza kwamba kwa msingi huo
wa Kikatiba ni vyema Wananchi wakafahamu na kuelewa kuwa Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Braza la Mapinduzi ataendelea kuwepo
madarakani mkapa pale Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar itakapomtangaza
mshindi wa kiti cha Urais na Rais Mteule atashika madaraka hayo baada ya
kuapishwa rasmi kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Katiba.
kutoka: http://bongocentral.blogspot.com
0 comments: