KIGOGO WA TCRA ASIMAMISHWA KAZI
Rais wa Tanzania
Dkt John Magufuli ameivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt Ally
Yahaya Simba.
Taarifa kutoka Ikulu imesema Bw Simba amesimamishwa
kazi kutokana na kutosimamia ipasavyo Mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa
usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS).
Bodi ya TCRA imekuwa ikiongozwa na Prof Haji Semboja.
Taarifa hiyo inasema hatua hiyo ilisababisha Tanzania kupoteza mapato ya takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka.
Mamlaka
ya Mawasiliano nchini (TCRA) iliingia mkataba na kampuni ya SGS juu ya
uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu tarehe 22 Machi,
2013.
Kampuni
hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano lakini mpaka sasa kampuni ya
SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na uthibiti wa
mapato ya simu za ndani (Offnet), kwa mujibu wa serikali.
Rais
Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi
Profesa Makame Mbarawa Mnyaa kumteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
hiyo mara moja.
Aidha, amewataka Waziri Prof Mbarawa, Katibu Mkuu
na Naibu Katibu katika wizara hiyo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa
ukusanyaji wa mapato ya simu kwa simu za ndani (Offnet) uanze kufanya
kazi, na nchi ipate mapato yanayostahili kukusanywa.
“Nataka
tukusanye mapato yote ya serikali yanayostahili na sitasita kuchukua
hatua dhidi ya yoyote atakayekwamisha jambo hili,” amesema Rais
Magufuli.
chanzo:bbcswahili
0 comments: