...................

ICC tayari kushauriana na Kenya kisheria


ICC inashikizwa iweze kuhamishia Kenya kesi za washukiwa William Ruto na Rais Uhuru Kenyatta

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya jinai ya kimataifa- ICC, Fatou Bensouda leo amesema kwamba mahakama hiyo iko tayari kushauriana na Kenya kisheria kuhusu ombi la kutaka kesi inayowakabili rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta na naibu wake, William Ruto kuhamishiwa nyumbani.
Tamko hilo linatolewa wiki moja tu baada ya viongozi wa Umoja wa Afrika kutoa wito kwa ICC irejeshe kesi za Uhuru na Ruto zishughulikiwe nchini Kenya.
Akijibu maswali ya waandishi kutoka radio moja ya kibinafsi ya Nairobi, mwendesha mashtaka huyo mkuu amenukuliwa akisema hatua ya ICC kufanya mazungmzo na Kenya kuhusu kesi za Uhuru na Ruto kurejeshwa nchini Kenya ni utaratibu wa kisheria utakao amuliwa na majaji wa ICC.
Alisema kwa mujibu wa mkataba wa Roma ambao ndio msingi wa mahakama ya ICC, nchi yoyote inayotaka kesi irejeshwe yafaa itosheleze kwa majaji wa ICC kwamba itaendeleza mashtaka hayo hayo kwa watuhumiwa.
Bi Bensouda alisema ICC ni mahakama huru ambayo haiegemei misingi ya kisiasa na majaji wake hutoa uamuzi bila kushurutishwa na yeyote.Alisema ICC itaendelea kushirikiana na mataifa 34 yaliyosaini mkataba wa kujiunga na mahakama hiyo.
Wiki jana, viongozi na serikali wanachama wa Umoja wa Afrika waliafikiana mjini Addis Ababa Ethiopia kwenye kongamano lao kwamba yafaa kesi zinazowakabili rais Uhuru Kenyatta, naibu wake, William Ruto pamoja na mwanahabari Joshua arap Sang zirejeshwe na kushughulikiwa nchini Kenya.
Uhuru na Ruto wameshtakiwa kwa kupanga na kufadhili mapigano ya baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya wa 2007, yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu na kuwaacha wengine takriban nusu milioni bila makao.

chanzo:bbcswahili
http://3.bp.blogspot.com/-e0QpO-QtZzE/U5DWDUZasXI/AAAAAAAABWg/QlFF97gwNdc/s1600/RAHA+GIF.gif
GIVE YOUR OPINIONS HERE

0 comments: