TAARIFA NZITO KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA HALI YA NCHI YETU
Msomi Bw Falesy Kibassa kutoka chuo kikuu cha Mzumbe Morogoro akizungumza na wahabari leo mjini Iringa huku akihimiza uzalendo zaidi katika Taifa
Wanahabari mkoani Iringa wakimsikiliza msomi Bw .Falesy Kibassa alipozungumza nao leo juu ya mambo mbali mbali
Wanahabari na wanazuoni wakimsikiliza msomi huyo leo
Wanahabari wa vyombo mbali mbali mkoani Iringa wakimsikiliza msomi huyo juu ya hali ya nchi yetu ilivyo kwa sasa
SIASA, UCHUMI, SHERIA, HAKI NA UWAJIBIKAJI
Wajibu wa Vijana, wasomi, wanasiasa na wataalamu
Utangulizi
Awali ya yote niwshukuru kwa mwitikio wenu kuja kunisikiliza na mwisho mtaniuliza maswali machache itakapolazimu.
Kwa majina naitwa FALESY KIBASSA,
kwa taaluma ni MHASIBU taaluma yangu ya kwanza kabisa ni MWANDISHI WA
HABARI kwa kazi ni MHADHIRI wa CHUO KIKUU MZUMBE kilichopo Mkoani
Morogoro. Mimi ni mkaazi wa Iringa, mzaliwa na mkulia Iringa KIHESA
SEMTEMA, nimesoma shule za Msingi Kihesa na Sekondari LUGALO.
Ni
Mtanzania halisi na nasimama hapa kwa haki na wajibu wangu kwa mujibu wa
katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho
yake yote kumi na moja (bila kuathiri mtiririko wake, ibara za 12 hadi
28 zinanipa haki na wajibu na kwa haki ya kutoa kupokea na kupata au
kutafuta habari ama taarifa zozote ibara ya 18 inanipa haki ya kuitisha
mkutano huu.
Pamoja
na kuwa mimi ni mwanachama wa chama cha siasa, lakini mimi si
mwanasiasa na sina nafasi yoyote ya kisiasa katika taifa hili.
Madhumuni ya mkutano huu
Nimewaiteni
ndugu waandishi kwa kujua kuwa sauti yangu itasambaa kwa kasi kubwa kwa
uwepo wenu na mkisaidia isambae badala ya kuzunguka na kuzungumza na
mmoja mmoja.
Kwa
kuwa mimi ni mkaazi wa Iringa na kwa wajibu na haki ya kiktaiba kama
mtanzania, nimeonelea ni vema tukazungumzia japo kwa ufupi masuala
kadhaa yanayohusu mustakabali kwanza wa mji wetu wa Iringa na pili wa
taifa letu hasa katika nyanja za SIASA na UCHUMI.
Tutayazungumzia
haya kwa kuangalia utii wa sheria na kanuni mbalimbali, haki ya kila
mwananchi na pia wajibu wake. Pia tutagusia japo kwa ufupi masuala
kadhaa hasa yaliyojitokeza siku za karibuni katika mji wetu.
Na
mwisho tutaweka matazamiao ya siku za baadae tutafanya nini ili kufikia
malengo ya kujipatia mafanikio ya KICHUMI na KISIASA.
Hali ya kiuchumi na kisiasa Iringa Mjini
Kwa
ujumla Iringa ni moja kati ya maeneo yaliyo na fursa za kukuwa kwa kasi
kiuchumi. Ongezeko la idadi ya watu ni fursa moja nzuri ya kuuwezesha
mji na mkoa kwa ujumla kupata maendeleo kwa kasi kubwa.
Kwa
hali ilivyo, Iringa ni bado mji maskini wenye pato la chini pamoja na
kuwa na ongezeko kubwa la watu kutoka wastani wa watu 106,000 mwaka 2002
hadi kufikia 151,000 mwaka 2012 karibu ongezeko la asilimia 50%.
Hi ni
changamoto kubwa ambayo kila mkaazi lazima aione kuwa moja ni fursa
lakini ni changamoto kama hali ya uchumi itakuwa haikuwi kwa kasi.
Pato
la Halmashauri ya manispaa ya Iringa lililoidhinishwa kwa mwaka wa fedha
2013/14 ni Tshs 21 bilion ikiwa ni wastani wa pato la kila mwananchi la
Tsh139,000 kwa mwaka Ukilinganisha na wastani wa lile la taifa la
Shilining 355,000.
Hii ni
kumaanisha iringa Mjini hata wastani wa Nusu ya Per Capita ya taifa
hatujafika (139,000/355,000). Hili ni suala la msingi ambalo kila
mwananchi lazima alione kuwa linamhusu.
Ukiona maeneo kama haya maana yake kuna watu wengi ambao ni maskini sana, zingatia hapa ni mjini.
Kuna
watu wanaohangaika kwa siku nzima kutafuta shiling 500 na Mungu saidia
apate kila siku anaweza kupata sh. 15,000 kwa mwezi.
Angalau
pato la kila mwana Iringa lingekuwa wastani wa sh. 500 kwa siku basi
ingekuwa pato la wastani kwa mtu mmoja (per capita income) ya sh 180,000
kwa mwaka na kwa wakaazi 151,000 basi ingekuwa pato la Halmashauri ni
Tsh bilioni 27 ambayo ni zaidi ya lile la sasa la bilioni 21.
Katika
takwimu za sensa ya watu na makaazi idadi kubwa ya watanzania ni vijana
inayokadiriwa kufikia asilimia 52 jambo ambalo liko wazi kuwa kwa mijini
ni zaidi ya hiyo inayofikia asilimia 60 hivyo hapa kuna changamoto
kubwa kwa vijana.
Hali ya kisiasa
Kwa
ujumla hali ya kisiasa Iringa bado ni tulivu. Kuna mambo machache na
madogo madogo ambayo ni sehemu ya changamoto za utendaji wa kila siku.
Kumekuwa na mivurugano ya hapa na pale na imetokea wiki iliyopita ambapo
kulikuwa na mvutano, msukumano na mfukuzano wa polisi na wananchi.
Sipendi
kulijumuisha kama linavyosemwa kama ilikuwa ni mapambano ya machinga na
polisi. Siyo kwamba nawatetea machinga wala nawasemea polisi la hasha
bali kulikuwa na mgongano wa maelewano kati ya machinga na amri halali
ya serikali lakini waliopambana na polisi si Machinga.
Machinga
ni wafanyabiashara duniani kote wanaoendesha uchumi wa miji. Kwa
takwimu zitokanazo na tafiti asilimia zaidi ya 55 ya uchumi wa Amerika
na Ulaya umetegemea wafanya biashara wadogo na kwa nchi kama Uholansi,
Denmark, Norway, Uingereza, Ufaransa na Canada, wafanyabiashara wadogo
ndio wanaotegemeza uchumi wa nchi hizo.
Tofauti ya maana ya wafanyabiashara ndogo ndogo kati ya Ulaya na Afrika ndiyo inayogomba.
Machinga
wa Ulaya wanatumia magari lakini machinga wa Afrika Tanzania hususani
wanatembea kwa miguu, mitaji ya waafrika na Asia na Latin Amerika ni
midogo sana ukilinganisha na wale wa Canada, Marekani, Ulaya na
Australia.
Sasa
wakati wafanyabiashara wadogo wanapambana kila siku kutafuta kujiongezea
mitaji kwa kufanya shughuli zao halali, kuna tatizo la kisiasa
linaloingia na kuingilia mifumo yote ya kiuchumi na kibiashara.
Hivyo
basi, kama vijana wasipokuwa makini kuweka balance ya mambo haya mawili
ya kiuchumi (kwa ajili yao) na kisiasa (kwa matakwa ya wanasiasa) basi
hali ya umaskini kwa taifa hili halitakaa liishe. Kuna wanasiasa
wanaochochea migogoro kwa maslahi yao binafsi na wala hakuna maslahi ya
watu.
Ifike
mahali watanzania na hasa vijana waachane na wanasiasa na badala yake
wajitume zaidi kwa kazi za kukuza uchumi wao kila siku na wakitaka
masuala ya siasa wafanye wenyewe kwa utashi wao.
Kusukumwa
na wanasiasa kwa kigenzo cha aina yoyote ama kwa kudanganywa au
kuvutwa, lazima vijana tupime maneno ya wanasiasa. Wanasiasa wengi
hawana weledi kwa wanayoyafanya isipokuwa wengi ni "waganga njaa".
Nieleweke
hapa naposema waganga njaa haijalishi ni wa chama gani wapo wengi sana
waganga njaa, wana maneno mengi matamu kuyasikiliza lakini hata wao
hawayaamini.
Hakuna haja ya kukaa na kuwasikiliza au kufuata yale wanayosema maana mwisho wa siku yatatupelekea kwenye uharibifu.
Mustakabali wa taifa letu
Tanzania
ipo na itaendelea kuwepo. Sisi sote tutaiacha Tanzania na hakuna aliye
mkubwa kuliko Tanzania. Jambo litakalotupeleka kwenye mustakabalu ulio
bora ni UZALENDO.
Tukizungumzia
dhana nzima ya Uzalendo tunazungumzia "Mapenzi na Uaminifu kwa taifa"
(The love for your country and loyalty towards it).
Hivyo
basi kama kila Mtanzania akiipenda nchi hii, akawa mwaminifu kwa nchi
hii, basi tutaitengeneza na kuijenga kwa manufaa ya sasa na vizazi
vijavyo.
Namna
yoyote ya kusukumwa kuiharibu hakutakuwa na nafasi miongoni mwetu iwe
kwa kijana ama mtoto ama mzee. Uzalendo wa vijana utalitegemeza taifa.
Changamoto
tunazozipata sasa, ni kuondokana na dhana ya uzalendo na "Umimi" na
"Usisi" kwa minajili ya "Ukombozi" vikitawala. Hii si sawa, haikubaliki
na wala haichukuliki.
Wanasiasa
wanasikika kila siku, wanasikilizwa sana lakini wameacha dhana ya taifa
na wameegemea kwenye maslahi binafsi. Wito wangu kwa watanzania,
tuwapuuze wanasiasa wanaotufundisha kuishi nje ya misingi ya uzalendo
maana tukishaachana na uzalendo hatutaupata tena.
Wito wangu kwa Vijana
Kwa
kuwa Tanzania ina vijana wengi. Na kwa kuwa vijana ndio wenye mbio na
wenye uwezo wa kudaka mambo mengi kwa muda mfupi na kuyafanyia kazi;
1.
Tuwaache wanasiasa na wana harakati za kisiasa wafanye harakati zao bila
kutuingiza katika majanga ambayo hata hawajui wakituingiza watatutoaje;
2. Adui
wetu wakubwa ni Umaskini, maradhi, huduma duni, miundombinu mibovu,
ukosefu wa mitaji, ukosefu wa maeneo salama kwa biashara zetu ndogo
ndogo na shida zinazotukabili za magonjwa na kuwa na mzigo wa kuhudumia
watu wengi wanaotutazama ambao ni wategemezi wetu.
Adui
wetu si CCM wala si CHADEMA wala si NCCR Mageuzi wala CUF wala TLP wala
chama chochote cha siasa, na Hivyo vyama vya siasa haviwezi kuwa Rafiki
zetu
3. Fikira zetu tuziongoze katika kukuza mitaji na kuendeleza mitaji midogo tuliyo nayo.
Wito wangu kwa wanasiasa
Kwa
kuwa mmetambua kuwa nguvu yenu bila vijana ni ndogo; na kwa kuwa
mumetambua kuwa hamuwezi kufanya siasa bila watanzania; na kwa kuwa
mnatambua kuwa Tanzania itaendelea kuwepo hata msipokuwepo; basi
nawasihi yafuatayo
1. Endesheni siasa kwa staha, weledi na utu. Msiwasukume wala kuwavuta watu kwenye masuala yaliyo kwa maslahi yenu binafsi
2. Nchi yoyote duniani inaendeshwa kwa falsafa kuu mbili moja SIASA na ya pili UCHUMI.
Hivyo mnapofanya siasa zenu basi waambieni watu jinsi ya kujiendesha kiuchumi.
3.
Muelewe kuwa, kwa nafasi mlizo nazo ni dhamana ambayo mumeipata bila
utaalamu wowote. Hivyo si kazi ya kudumu ingawa wengine mwataka kuifanya
ya kudumu.
Kwa
kuwa wanasiasa ndipo mnapata fursa ya kuendesha mifumo ya kiuchumi.
Itumieni dhamana mliyopewa kwa faida ya taifa na si faida yenu.
4.
Katika misuguano yenu ya kisiasa, msitafute huruma ya wananchi kwa
kuomboleza kwao. Mnalo jukumu la kuwashawishi lakini si kwa kulazimisha
matakwa yenu sasa.
Jifunzeni kutengeneza falsafa ambayo taifa litakaa nazo hata mtakapokuwa hampo.
Leo
tunapomkumbuka Mwalimu Nyerere si kwa sababu tu alikuwa Rais wa kwanza
wa Tanganyika huru na Tanzania Jamhuri bali kwa sababu ya falsafa yake
kuu ya UMOJA wa Taifa. Jiulize wewe leo una falsafa gani.
Wito kwa wasomi na wataalamu wa taifa hili
Kwa
kuwa nchi inaendeshwa kwa falsafa ya UCHUMI na SIASA. Uchumi ni taaluma
ya matumizi ya raslimali za taifa kwa kuzingatia kuwa raslimali daima ni
chache kuliko uhitaji isipokuwa hewa.
Kwa
hiyo dhana kubwa inayotawala uchumi ni UCHAGUZI (CHOICE) wa nini ufanye
na Nini uache ambacho huwa ni Ghalama halisi (OPPORTUNITY COST) ya kile
unachofanya.
Raslimali
kuu ambazo kila taifa linazo ni WATU, ARDHI na MITAJI. Ndipo ili
Raslimali hizi ziweze kufanya kazi kwa ufanisi unahitaji SIASA SAFI NA
UONGOZI BORA.
Tunapozungumzia
UONGOZI BORA siyo wa watu tu bali wa hizi tatu zote na hii ndiyo dhana
ya UJASIRIAMALI ama wanaita "ENTREPRENEURSHIP".
Kwa
kuwa wataalam na wasomi mnao uelewa mpana juu ya masuala haya; na kwa
kuwa man wajibu kwa taifa hili; basi wito wangu ni huu;
1.
Tumieni utaalam wenu kwa manufaa ya watanzania na pia toeni vipawa vyenu
bure hasa kwa vijana maana wapo waliowapa huo utaalamu bure kabisa na
nyie toeni bure;
2.
Wataalamu washaurini wanasiasa kitaalamu ili kwa mustakablia wa taifa
falsafa hizi mbili za UCHUMI na SIASA ziende sawa. Ukiwa mtaalamu halafu
ni mwoga mbele ya wanasiasa basi na utaalamu wako ni hasara kwa taifa.
3.
Vijana wasomi hasa mlioko vyuoni sasa; achaneni na ushabiki wa kisiasa
maana ushabiki huo hauna tija kwa taifa. Tumieni muda wenu mwingi
kujifunza mifumo mbalimbali ya kiuchumi duniani badala ya kukaa na ama
kusifia ama kuponda vyama vya siasa.
Wito kwa waandishi wa habari na taasisi zake
Kwa
kuwa vyomba vya habari ndivyo muhimili mkubwa wa kupasha habari na
kupeana taarifa za kila siku; na kwa kuwa kwa Tanzania kuna maendeleo
makubwa ya technolojia ya habari na uanahabari; na kwa kuwa mimi
nayezungumza nanyi ni mwanazuoni mwenzenu; basi wito wangu kwenu ni huu.
Tumieni
kalamu zenu, kamera zenu, vinasa sauti vyenu na mitambo yenu kwa ajili
ya kupeleka habari zenye manufaa kwa taifa. Kila habari ni habari lakini
si kila habari inafaa kuripotiwa. Ushabiki wa aina yoyote si sehemu ya
taaluma.
Nchi
zote zilizowahi kuwa na machafuko na mapigano ya wao kwa wao, kuna
baadhi ya waandishi waliokuwa ni chachu ya mapigano hayo. Mfano mzuri
mnaufahamu ni yale mauaji ya Kimbari kule Rwanda mwaka 1994.
Si
jambo jema kwa waandishi wa habari kushabikia uvunjifu wa sheria, au
kuwa na msimamo kwa jambo lolote lenye utata hasa kwenye jamii yetu
yenye kundi kubwa la vijana
Mwisho
Taifa
hili linatuhitaji sisi sote ili lipate maendeleo. Hivyo hatuna budi
kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo yetu binafsi na mwisho
kutakuwa na maendeleo ya jumla.
Kumbuka
hatuwezi wote kuwa wanasiasa ama hatuwezi wote kuwa wafanyabiashara ama
hatuwezi wote kuwa waandishi ama wote kuwa wataalamu.
Tumegawanyishwa ili kuweza kufaidiana. Lakini cha kujilinda ni
kusukumwa na wanasiasa na kufikia hatua ya kufanya uhalifu kwa kisingizio cha
ukombozi, hizo ni siasa za MAJI TAKA ambazo zitaliangamiza taifa.
Kuna watu wanasema wanafanya hayo kwa sababu hawana cha
kupoteza, ndugu zangu tusijidanganye maisha ni kila kitu hivyo usijaribu
kuyachezea etu huna cha kupoteza. Ikiwa unaona huna cha kupoteza, jaribu
Kujikata kidole.
Asante kwa
kunisikiliza!
Mungu IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI IRINGA
chanzo:Francis Godwin
0 comments: