Hatimaye Afghanistan yakabidhiwa majukumu ya usalama wake

...................
Hatimae vikosi vya Afghanistan vimekabidhiwa rasmi uongozi wa majukumu ya usalama wa nchi nzima kutoka kwa vikosi vya Kimataifa. Nato imeitaja hatua hiyo kama ni mwanzo wa kuendelea mbele kwa nchi hiyo
Rais Hamid Karzai wa nchi hiyo akizungumza katika sherehe ya ukabidhi wa majukumu hayo hii leo tarehe 18.06.2013 iliyofanyika katika shule ya mafunzo ya kijeshi ya Afghanistan nje ya mji wa Kabul amesema sasa majukumu ya usalama yatakuwa mikononi mwa vikosi vya nchi hiyo. Hata hivyo shughuli hiyo imesadifu na shambulio la bomu magharibi ya Kabul.
Shambulio hilo la bomu limetokea muda mfupi kabla ya sherehe za kukabidhi majukumu ya usalama kwa jeshi la Afghanistan kutoka kwa jeshi la kimataifa.Kiasi watu watatu wameuwawa na wengine 21 wakajeruhiwa kufuatia shambulio hilo ambalo limeongeza wasiwasi juu ya vipi jeshi la Afghanistan litaweza kukabiliana na uasi unaoongozeka baada ya vikosi vingi vya kigeni kuondoka nchini humo kufikia mwishoni mwa mwaka 2014.
Msemaji wa wizara ya ndani Sediq Sediqqi amesema mripuko huo umetokea wakati msafara wa mwanasiasa maarufu na ambaye pia ni kiongozi wa kidini Mohamad Mohaqiq ulipopita katika eneo hilo.Mwanasiasa huyo pia ni mwanachama mkuu katika baraza lililoundwa na rais Karzai mwaka 2010 ya kujaribu kutafuta makubaliano ya amani na Wataliban.
Rais Karzai hata hivyo amesema wanajeshi wa nchi yake sasa wanayabeba majukumu kamili ya usalama wa taifa hilo linalokumbwa na vita kutoka kwa jeshi la shirika la kujihami la Nato linaloongozwa na Marekani.
Jeshi la Nato kuondoka
Shughuli hiyo ya ukabidhi wa majukumu ya usalama ni hatua muhimu katika kipindi cha takriban miaka 12 ya vita na inaanzisha pia mwanzo mpya kwa Marekani na vikosi vya NATO kwa ujumla ambavyo sasa vitahusika tu katika jukumu la kusaidia na kufungua njia ya kuondoka kabisa kwa jeshi hilo ndani ya kipindi cha miezi 18 ijayo.
Katibu mkuu wa Nato Anders Fogh Rasmussen amesema jeshi la Natolitatoa msaada wa kijeshi ikiwa litahitajika lakini haliweka tena mipango ya kuchukua majukumu hayo,´au kuongoza shughuli hizo.
Rais Obama na katibu mkuu wa Nato Rasmussen Rais Obama na katibu mkuu wa Nato Rasmussen
Baada ya shughuli hiyo ina maana sasa njia iko wazi ya wanajeshi kiasi 100,000 kutoka nchi 48 ikiwemo 66,000 wa kimarekani kuondoka nchini Afghanistan.Kufikia mwishoni mwa mwaka huu wanajeshi nusu wa jeshi hilo la NATO watakuwa wameondoka na kufikia mwishoni mwa mwaka 2014 wanajeshi wote wanatazamiwa kuwa wameondoka na mahala pao kujazwa na kikosi kidogo kitakahusika kutowa mafunzo na ushauri endapo serikali ya Afghanistan itaidhinisha hatua hiyo.
Rais Hamid Karzai ameitaja hatua hiyo ya kukabidhi majukumu ya kulinda usalama kuwa ya kihistoria kwa nchi yake na juu ya hilo amechukua nafasi hiyo kutangaza rasmi juu ya kuanza mazungumzo na wataliban.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri Mohammed AbdulRahman.

Na dw swahili
http://3.bp.blogspot.com/-e0QpO-QtZzE/U5DWDUZasXI/AAAAAAAABWg/QlFF97gwNdc/s1600/RAHA+GIF.gif
GIVE YOUR OPINIONS HERE

0 comments: