Marekani yatoa ripoti kuhusu Ugaidi duniani

...................

Matukio ya Kisiasa

Marekani yatoa ripoti kuhusu Ugaidi duniani

Marekani imeishutumu Iran kwa kuongeza ufadhili wa shuguli za kigaidi mwaka jana kwa kiwango ambacho hakijashuhudiwa kwa karibu muongo mzima huku mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda ukipoteza ngome zake..
Hayo yametajwa kwenye ripoti ya Marekani ya kila mwaka kuhusu hali ya ugaidi kote duniani.Katika ripoti iliyowasilishwa katika bunge la Marekani,wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeendelea kushikilia msimamo wake kuzihusu nchi nne Cuba,Iran,Sudan na Syria kama mataifa yanayofadhili ugaidi jambo ambalo linaambatana na vikwazo vikali.
Ripoti hiyo inasema kuwa ufadhili wa Iran wa shughuli za kigaidi ulishuhudiwa kuongezeka mwaka jana kwa kiasi ambacho hakijashahudiwa tangu miaka ya 90, ikiangazia shuguli za Iran na inavyounga mkono kundi la wanamgambo la Hezbollah lenye makao yake nchini Lebanon huku mashambulio yakipangwa kusini mashariki mwa Asia,Ulaya na Afrika.
Hezbollah lahusishwa na ugaidi
Kundi la Hezbollah limehusishwa na shambulio la bomu la mwezi Julai mwaka jana nchini Bulgaria ambalo raia watano wa Israel na raia mmoja wa Bulgaria waliuwawa na wengine 32 kujeruhiwa.Vile vile kumekuweko na madai ya kuhusika kwao katika njama dhidi ya Cyprus na Thailand.
Wizara hiyo ya mambo ya nje ya Marekani pia imezikosoa Iran na Hezbollah kwa kumsaidia Rais wa Syria Bashar al Assad katika ukandamizaji wake wa kinyama dhidi ya waasi wanaotaka kumng´oa madarakani.
 Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah
Ripoti hiyo inakuja huku umoja wa ulaya ukitafuta kuliorodhoesha kundi la Hezbollah kama kundi la kigaidi kufuatia maombi ya kufanya hivyo kutoka Marekani na Israel.Hezbollah ni kundi lenye nguvu kubwa kisiasa na la wanamgambo katika nchi ya Lebanon.
Wakati huo huo Marekani imesema nguvu ya mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda ziko katika njia ya kushindwa na kwamba mtandao huo uliokuwa ukiongozwa na Marehemu Osama bin Laden umeanza kutetereka kutokana na operesheni madhubuti inayoongozwa na Marekani nchini Pakistan.
Al Qaeda yapoteza makali yake
Kutokana na kupoteza wengi wa viongozi wake wakuu, Al Qaeda imepoteza uwezo wake wa kupanga shughuli zake na kufanya mashambulizi kwani viongozi waliosalia wanazingatia mno sasa jinsi ya kujinusuru.
Ripoti hiyo imetetea uamuzi wake wa kuendelea kuiweka Cuba katika orodha ya nchi zinazotajwa kufadhili shughuli za kigaidi kwa kusema Kisiwa hicho kinatoa hifadhi kwa wanachama wa kundi la waasi wa ETA wanaopigania kujitenga jimbo la Uhispania la Basque pamoja na waliotoroka ambao wanasakwa na Marekani.
Osama bin Laden Osama bin Laden
Hao ni pamoja na Joanne Chesimard anayetuhumiwa kwa kumuua afisa wa polisi miaka 40 iliyopita ambaye shirika la upelelezi la FBI mapema mwezi huu lilimuorodhesha miongoni mwa magaidi wanaosakwa zaidi.Marekani imekuwa ikiitenga Cuba taifa la kikomunisti tangu Fidel Castro aliponyakuwa madaraka mwaka 1959.
Huku ikiripotiwa kufanyika kwa mashambulio ya kigaidi katika nchi 85 mwaka jana,asilimia 55 ya mashambulio hayo na asilimia 62 ya vifo vilivyotokana na mashambulio hayo yalifanyika katika nchi tatu;Pakistan,Iraq na Afghanistan.
Ripoti hiyo ya Marekani inasema kulikuwa na mashambulio ya kigaidi 6,771 mwaka jana ya ambapo watu 11,098 waliuawa na zaidi ya 1,280 walitekwa nyara.
Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa/Reuters
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman 

Kutoka Dw swahili
http://3.bp.blogspot.com/-e0QpO-QtZzE/U5DWDUZasXI/AAAAAAAABWg/QlFF97gwNdc/s1600/RAHA+GIF.gif
GIVE YOUR OPINIONS HERE

0 comments: