TUNDU LISSU ALONGA JUU YA KICHAPO WALICHOPATA
Mbunge wa Singida Mashariki,Tundu Lissu akiwaonyesha waandishi wa habari
miwani yake aliyodai kuvunjiwa na polisi. Lissu alipata dhamana katika
Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati, jijini Arusha jana baada ya kukamatwa
juzi.
Wabunge wanne wa Chadema, ambao waliachiwa na polisi kwa dhamana
wamesimulia mateso waliyoyapata wakiwa rumande baada ya kukamatwa juzi.
Vigogo hao; Mbunge wa Mpanda Mjini Said Amour
Arfi, Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce
Mukya (Viti maalumu), walikamatwa juzi baada ya wao na wafuasi wa chama
hicho kutawanywa kwa mabomu ya machozi na polisi kwenye Viwanja vya
Soweto, Arusha.
Wabunge hao waliachiwa baada ya kujidhamini
wenyewe huku watu wengine 65 waliokamatwa pamoja nao wakiachiwa baada ya
kudhaminiwa.
Wote wanatakiwa kuripoti kwenye kituo hicho Julai 22, mwaka huu na wataelezwa hatma ya suala hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa
Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema jeshi lake
linaendelea kuwasaka Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na
Mbunge wa Arusha, Godbless Lema na kuwaonya kuwa wanatakiwa
kujisalimisha mara moja.
Chagonja alisema Mbowe na Lema wanatafutwa kwa
kosa la kufanya kusanyiko lisilo halali katika viwanja hivyo vya Soweto
walipokuwa wakitaka kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi,
Ramadhan Juma na Amir Ally waliofariki dunia baada ya kuumizwa kutokana
na mlipuko wa bomu, Jumamosi iliyopita.
Pia aliwaamuru Mbowe na Lema kuwasilisha mara moja
ushahidi wa kuwahusisha polisi na shambulio la bomu na kama hawana
imani na Polisi, basi wawasilishe ushahidi wao kwa Rais Jakaya Kikwete.
Lissu
Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni, alilalamikia kitendo cha polisi kumwagia maji ya
kuwasha baada ya kumkamata.
“Walinimwagia maji ya kuwasha kwa mfululizo
nikalazimika kulala chini kifudifudi huku nikiwa nimefunika macho
kukwepa yasiingie maji. “Kuna askari walitaka kunipiga lakini
niliokolewa na mwenzao mmoja aliyenikinga nisishambuliwe. Kwa kweli
ilikuwa hali ya hatari,” alisema.
Alisema polisi hao waliomkamata walivunja miwani yake kwa makusudi akisema aliikabidhi kaunta ikiwa haijavunjika.
“Wakati naingia mahabusu nilikabidhi miwani yangu
lakini ajabu wakati tukiachiwa ilikuwa imevunjika.” Alilalamikia hatua
ya polisi kuwashambulia kwa mabomu, kuwamwagia maji ya kuwasha
walipokuwa wakiwatawanya watu waliokusanyika Soweto akisema awali,
waliwaruhusu.
“Kwa maoni yangu na maoni ya wenzangu, hakukuwa na sababu ya
polisi kupiga mabomu, risasi na kumwagia watu maji ya kuwasha kwani ni
wao ndiyo walituomba tubebe dhamana ya uongozi kwa kwenda kuwaomba
wananchi waliokusanyika pale uwanjani kutawanyika,” alisema Lissu.
Alisema Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD),
Gilles Mroto ndiye aliyewaruhusu kuzungumza na wananchi ili watawanyike
baada ya viwanja hivyo kuzuiwa kutumika kwa shughuli ya kuaga miili ya
waliopoteza maisha kwenye tukio la bomu.
Alisema pamoja na ruhusa hiyo, polisi waliwaruhusu
Chadema kuchukua magari yao yenye vipaza sauti ili wavitumie
kuwatawanya wananchi hao lakini ajabu polisi ikawapiga mabomu mara baada
ya Arfi kuwataka wananchi watawanyike kwenda Hospitali ya Mount Meru
kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.
“Kama ule mkusanyiko haukuwa halali, kwa nini
polisi haohao walikaa na wananchi wale tangu asubuhi na wakaturuhusu
kuzungumza nao ili watawanyike?”
Alisema kisheria, mkusanyiko usio halali
unastahili kusambaratishwa kwa mabomu baada ya polisi kutoa ilani kwa
wahusika kutawanyika tofauti na juzi akisema hawakutoa ilani yoyote.
Akunaay
Akunaay alisema polisi wanapaswa kubadilisha mbinu
za kukabiliana na watu wanaodhani wamevunja sheria badala ya kukimbilia
kupiga mabomu na kufyatua risasi.
“Mabomu na risasi ni kukomaza watu na kuwafanya
wazoee milipuko. Itafikia hatua wananchi watajenga usugu na kuanza
kupambana na polisi,” alisema na kuongeza:
“Polisi baada ya kutukamata na kutuweka chini ya
ulinzi walitupiga hadi tukiwa kituoni bila sababu yoyote. Nadhani askari
wetu wanapaswa kuacha kumalizia hasira zao za magumu yao yanayowakabili
kwa kuwapiga watuhumiwa.”
Mukya
Mukya amelalamikia kitendo cha polisi kukataa
kumpa fursa ya kumnyonyesha mtoto wake mchanga akisema malaika huyo
alilazimika kushinda njaa kutwa nzima ya juzi na usiku kucha.
“Niliwaomba polisi wanikubalie kujidhamini au
wanisindikize nikamnyonyeshe mtoto lakini walinikatalia kama vile
ninakabiliwa na kesi ya mauaji,” alisema Mukya.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyeki wa Baraza la Wanawake wa
Chadema (Bawacha), Susan Lyimo alisema: “Ni kinyume cha taratibu za haki
za binadamu kwa mwanamke kunyimwa nafasi ya kunyonyesha mtoto wake.”
Polisi wajibu
Akizungumzia malalamiko ya wabunge hao, Kamishna
Chagonja alisema hakuna mtuhumiwa ambaye anaweza kutoka mahabusu
akaimwagia sifa kwa sababu siyo mahali pa kusifiwa, bali ni mahali penye
kizuizi cha muda ili kuwezesha mkondo wa sheria kuchukua nafasi yake.
“Hatuna (polisi), roho ya Adolph Hitler (dikteta
wa zamani wa Ujerumani), tupo kwa ajili ya kulinda wananchi na mali
zao,” alisema.
Aidha, alikanusha madai ya Mukya ya kunyimwa
ruhusa ya kumnyonyesha mwanaye akisema: “Siku hizi kuna dawati la jinsia
katika vituo vyetu vya polisi kwa hiyo kama ni kunyonyesha lazima
wangesimamia utaratibu wa kumwezesha kufanya hivyo, siyo kweli kwamba
amekataliwa, haya ni maneno ya kulichafua jeshi.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
alisema wanaojihusisha na uhalifu wowote huwa na imani kuwa watafanikiwa
kujificha au kukwepa mkono wa dola na inapotokea wamekamatwa na
kuchukuliwa hatua, huanza kujitetea kwa kuwashushia lawama polisi.
“Hasa wanasiasa na wanaharakati wakikamatwa na
kuwekwa rumande, wengi hutoa manung’uniko mengi yakiwamo ya uongo,
ilimradi kuchafua polisi mbele ya wananchi. Hatupo kwa ajili ya
kusifiwa, bali kutimiza wajibu wetu,” alisema Sabas.
Kifo chaongezeka
Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na
mlipuko huo imefikia wanne baada ya mtoto Fahad Jamal (7), aliyekuwa
amelazwa katika Hospitali ya Seliani kufariki dunia jana. Kaimu
Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Paul Kisanga alithibitisha jana kufariki
kwa majeruhi huyo aliyekuwa ameumia kichwani na kulazwa kwenye chumba
cha wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU).
Mmoja kuagwa leo
Kiongozi wa Chadema, Judith Moshi aliyefariki
kwenye tukio hilo la bomu, leo anatarajiwa kuagwa kwa heshima zote za
chama hicho katika moja ya makanisa jijini Arusha baada ya polisi
kukizuia chama hicho kuendesha shughuli hiyo katika eneo la wazi.
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chadema,
John Mnyika alisema baada ya kuagwa, marehemu Moshi atazikwa Arusha
badala ya kusafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro kama ilivyokuwa
imepangwa awali ili kutoa fursa kwa wananchi wa jiji hilo kushiriki
katika mazishi yake.
“Kanisa gani na makaburi yapi tutamuagia na kumzika marehemu,
tutatangaza baadaye au kesho asubuhi baada ya mashauriano kati ya
viongozi na ndugu wa marehemu ambaye atazikwa kwa heshima zote za
chama,” alisema Mnyika.
Awali, marehemu Moshi alitarajiwa kuagwa kwenye
Viwanja vya Soweto kabla ya kusafirishwa kwenda Kilimanjaro lakini Jeshi
la Polisi lilizuia shughuli hiyo kufanyika kwenye viwanja hivyo baada
ya kupokea maelekezo kutoka kwa wamiliki wake ambao ni Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Mwananchi
Mwananchi
0 comments: