"WAASI WA M23 WAKITAKA VITA SISI TUPO TAYARI".....JWTZ .

................... http://www.ippmedia.com/media/picture/large/tyt(1).jpg Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa onyo kwa kikundi cha waasi nchini Kongo cha M23, kuwa kikiwachokoza lipo tayari kwa vita.

Kauli hiyo imetolewa na msemaji wa jeshi hilo, Kanali Kapambala Mgawe, wakati akihojiwa na NIPASHE Jumamosi kutokana na tishio lililotolewa na kikundi hicho kuvamia mji wa Goma endapo Serikali ya Kongo itajiondoa kwenye mazungumzo ya amani.

Kanali Mgawe, alisema wanajeshi waliopiga kambi eneo la Goma, wamejitayarisha kwa vita ya aina yoyote, na hawatasita kutoa kipigo kikali baada ya kuona kikundi hicho cha M23 kinawashambulia.

Wanajeshi wa Tanzania wapo nchini humo kuunda kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa ambacho kimepewa jukumu la kunyang'anya silaha waasi pamoja na kulinda amani mashariki ya nchi hiyo.

Nchi zingine zilizopeleka majeshi yao kuunda kikosi hicho ni Malawi na Afrika ya Kusini.

Hata hivyo, kwa siku za hivi karibuni hali ya amani katika mji wa Goma imezidi kuzorota, huku Mashirika ya habari ya Kimataifa yakieleza wanajeshi wa kikundi hicho wapo karibu na mji huo na kuongeza hali ya wasiwasi kwa wananchi.

"Jeshi lipo na hali nzuri, hatuna hofu na vitisho vya waasi kwa sababu tumejiandaa kwa kila kitu, ni wazi waasi wakitushambulia watakuwa wendawazimu, tutajibu kwa makali ya hali ya juu,
" alisema Kanali Mgawe.

Alisema hawana sababu ya kuingilia vita hiyo kwa sasa kutokana na utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa kuwapa kazi ya usuluhishi, kabla ya kutumia nguvu kama wakiona haki ya kimsingi ya wananchi inakiukwa.

"Kuna mambo kadhaa hatujakamilisha katika uundaji wa kikosi cha Umoja wa Mataifa, lakini tumeanza kufanya kazi ya kuchunguza na kupata taarifa zinazoweza kutusaidia tukianza kazi rasmi," aliongeza.

"Watanzania wasiwe na wasiwasi, vijana wetu wana mafunzo na zana za kisasa za kuwafanya kuwakabili waasi ambao wengi wameokotwa mitaani na hawana mbinu za kivita."

Alisema, hali ya mji huo ipo tulivu, ingawa katika siku za hivi karibuni waasi wa kikundi cha Maimai walivamia gereza moja na kuwatorosha wafungwa ili kuwalazimisha kujiunga na kikundi hicho.


chanzo:gumzo la jiji
http://3.bp.blogspot.com/-e0QpO-QtZzE/U5DWDUZasXI/AAAAAAAABWg/QlFF97gwNdc/s1600/RAHA+GIF.gif
GIVE YOUR OPINIONS HERE

0 comments: