Mzimu wa Escrow: mwingine asimamishwa akimfuata Tibaijuka
Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue, amemsimamisha kazi kwa muda ,
Eliakim Maswi, Katibu Mkuu ya Wizara ya Nishati na Madini, ili kupisha
uchunguzi wa tuhuma dhidi yake, kama ilivyoelekezwa na Rais wa Tanzania,
Jakaya Mrisho Kikwete.
Balozi Sefue amemsimamisha kazi Ndugu
Maswi kuanzia , Jumanne, Desemba 23, 2014, kwa kutumia madaraka
aliyonayo kama Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na
Rais, wakiwemo Makatibu Wakuu.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya
Balozi Sefue mjini Dar es Salaam imesema kuwa amechukua hatua hiyo “Kwa
mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Na. 8 ya
mwaka 2002 (kama ilivyorekebishwa)”ambapo “Katibu Mkuu Kiongozi ndiye
Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwemo
Makatibu Wakuu.
Badala yake, Balozi Sefue amesema kuwa Naibu
Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi C. Mwihava
atakaimu nafasi ya Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, hadi
uchunguzi dhidi ya Ndugu Eliakim C. Maswi utakapokamilika.Taarifa hiyo
ya Balozi Sefue pia imekariri kauli ya Rais Kikwete katika hotuba yake
kwa Taifa jana, Jumatatu, Desemba 22, 2014 ambako Rais alisema:
“Kuhusu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni Mtumishi wa
Umma, anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma, hivyo
nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana
makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa.”
Ndugu Maswi, aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu Ndugu Frederick Werema pamoja na Mawaziri wawili
walituhumiwa wakati wa Kikao cha Bunge kilichopita kuhusiana na Akaunti
ya Tegeta Escrow.
chanzo:bbcswahili
0 comments: