Nchi za Afrika Mashariki zaadhimisha siku ya mazingira duniani. :
Watoto wa shule wakikusanya taka baharini huko Karachi Pakistan ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya mazingira duniani.
Mwaka wa 1972, umoja wa mataifa ulitenga tarehe tano mwezi wa sita kuwa siku ya mazingira ambayo inatilia mkazo umuhimu wa kuhifadhi mazingira ili kupunguza madhara yanayoleta mabadiliko ya tabia nchi.
Lengo la jambo hili ni kuhakikisha kuwa kizazi cha sasa kinatumia mazingira kwa njia inayofaa ili vizazi vijavyo navyo visaidiwe.
Kwa mujibu wa takwimu za shirika la serikali la hesabu nchini Uganda, asili mia 48 ya waganda hawapati lishe bora huku asilimia sita wakiwa hawana uhakika kuwa watapata angalau sahani moja ya chakula kila siku.
Hii ni kwa sababu ya matumizi mabaya ya mazingira ambayo yamesabisha mmomonyoko wa udongo, mafuriko na jua kali miongoni mwa madhara mengine.
Waziri wa mazingira Ephraim Katuntu akizungumza kwenye sherehe hizi za mazingira, ujumbe wake aliamua kuuwasilisha kwa kuirejelea bibilia.
"Mungu aliumba mbingu na nchi na alipoziangalia akaona zinavutia. Aliumba mito na bahari na akaona zilikuwa murua kabisa. Aliendelea na hatimaye akamuumba mwanadamu. Litafakari hilo".
Mungu hakumuumba biandamu kwanza. Alimuumba wa mwisho na kumwamrisha alinde vyote ambavyo alikuwa ameviumba, kwa hivyo mwanadamu kuharibu kile Mungu alichoumba na kusema kilikuwa kizuri na kuhakikishia hautaingia mbinguni.
Wilaya ya Kalangala ambako sherehe za leo zilifanyika ipo katikati ya ziwa Victoria na ina visiwa 84. Sherehe, zilifanyika kwenye kisiwa cha Ssese ambacho wakazi wake wanasema ni kisiwa cha amani, ufanisi na minazi.
Kisiwa hiki kinasifika sana kwenye kilimo cha minazi. Hapo awali, wakazi wengi wa eneo hili walivua samaki kama njia ya kipekee ya kujikimu ki-maisha lakini kuanzia mwaka wa 2006, hali hii imebadilika. Serikali iliwashinikiza waanze kilimo cha minazi ambayo inatumika kutengeneza mafuta.
Ni mradi ambao umefua dafu sana kwa sababu wakulima 1,600 ambao hapo awali hawakuwa na kipato sasa hivi wanapata pesa zisizopungua dola mia moja kila mwezi.
Hii ni mojawapo wa sababu ambayo shirika la kulinda mazingira nchini Uganda - NEMA likachagua sherehe za mwaka huu ziadhimishiwe wilayani Kalangala. Mwandishi wetu wa Kampala Leyla Ndinda alizungumza na Nelson Bassalidde meneja wa shirika linalowashauri wakulima njia kuhusu njia bora za kulima na kulinda mazingira nikitaka kujua ni vipi wameweza kulinda mazingira licha ya kuwa walikata miti mingi wakati wakitengeneza mashamba ya kupanda minazi.
Na huko Kenya siku hiyo imeadhimishwa kwa kampeni mbali mbali za utunzaji mazingira . Mary Mgawe amezungumza na Wanjiru Mathai mwenyekiti wa taasisi ya mazingira katika chuo kikuu cha Nairobi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mpiganaji wa harakati za mazingira nchini Kenya Wangari Mathai.
Na huko Tanzania siku hiyo imeadhimishwa mkoani Rukwa kwenye kijiji cha Namanyere na kuzinduliwa kampeni rasmi za kimazingira. Mary Mgawe amezungumza na mkuu wa mkoa wa Rukwa kuhusu maadhimisho nchini humo.
Kutoka VOA swahili
0 comments: