ZIFAHAMU NJIA 9 ZINAZOASHIRIA MWISHO WA DUNIA

...................




Imeandaliwa na MaendeleoVijijini Blog
WENGI wanapoambiwa kwamba mwisho wa dunia, yaani kiama, utafika, mara nyingi hawaamini na wanaona ni kawaida kwa sababu watu wanazaliwa wengine wanakufa.
Wapumbavu wamefikia hatua ya kukufuru wakisema kwamba mwisho wa dunia ni pale unapokufa tu, siyo zaidi ya hapo huku wakisadiki tafiti za kisayansi ambazo mara nyingi zinapingana na uwepo wa Mungu.
Wengine utawasikia wakisema; “Tangu enzi za mababu na mababu tumeambiwa kuna mwisho wa dunia, Wakristo wanaamini Yesu atarudi, na waumini wa dini nyingine nao wanaamini kuna kiama, lakini mbona hatuuoni huo mwisho wa dunia?”

Hata hivyo, MaendeleoVijijini inaripoti bila shaka kuwa, zipo baadhi ya tafiti ambazo zimebainisha kwamba mwisho wa dunia umekaribia.
Matukio ya sasa yanayotokea ulimwenguni, majanga, vita, mabaa ya njaa, magonjwa ya ajabu na kadhalika ni dalili tosha kwamba mwisho wa dunia umekaribia.
Tafiti mbali mbali za kisayansi nazo zinaashiria hivyo kama ilivyoandikwa kwenye Vitabu Vitakatifu. Sayansi na teknolojia imeleta mabadiliko makubwa ambapo hivi sasa dunia ipo kiganjani, wengine wanasema ni kama kijiji tu.
Leo hii watu hawatembei na Biblia wala Qur’an, bali wanavipata vitabu vyote kupitia kwenye simu zao za viganjani. Suala la kununua vitabu linaonekana ni la kale sana, hakuna anayejisumbua kwenda kuuliza bei, achilia mbali kununua. Hii inatokana na mafanikio makubwa ya tafiti za kisayansi na kiteknolojia.
Lakini hebu jiulize, siku mitambo hiyo ya internet itakapozima hali itakuwaje? Hiyo tafsiri yake ni rahisi sana, kwani itasadifu Maandiko Matakatifu kwamba hata Neno la Mungu halitaonekana wala kupatikana tena. Si Biblia wala Qur’an ambazo zitakuwepo kwa sababu hata mitambo ya kuchapa vitabu hivyo hivi sasa inaweza kufungwa kutokana na kuingia hasara!
Hata hivyo, wanajiografia na mambo ya sayansi wameeleza mambo yaliyodhahiri yanayotokea hivi sasa kama ni viashiria vya mwisho wa duniani, hebu soka hapa:
Hollywood vs. Uhalisia

Majanga ya mabadiliko ya tabianchi na viumbe vya ajabu vyenye sura za kutisha (aliens) ndivyo vitu ambavyo vimechukua sehemu kubwa ya filamu za Hollywood vikiashiria mwisho wa mwanadamu katika sayari ya Dunia.
Kwa hakika, kuanzia filamu ya miaka ya 1950 ya "The Day the Earth Stood Still" hadi filamu ya miaka ya 1960 ya "Planet of the Apes" mpaka filamu za sasa kama "The Day After Tomorrow," na "After Earth," kiama kimedhirika katika hadithi za kufikirika zinazoashiria uhalisia.
Lakini najua kwamba, ingawa filamu hizi zinaweza kuwa za kufikirika na kufurahisha tu, wanasayansi wengi wana hofu kubwa kutokana na matukio yanayoendelea kutokea kila kukicha — mengine yakiwa mabaya kuliko hata yale yanayoonekana kwenye filamu.
Kutoka kwenye magonjwa ya kutisha ya kuvu (fungus) hadi ujio wa maroboti, kuna mabo tisa hapa ambayo wanasayansi wanayaona kwamba ni dhahiri kuhusu mwisho wa dunia.
Kuongezeka kwa joto duniani 
Mabadiliko ya tabia nchi ndiyo mama wa hofu zote za mwisho wa dunia, kwa sababu ndilo tishio kubwa linaloikabili dunia kwa sasa, kama wanavyosema wanasayansi wenyewe.
MaendeleoVijijini ambayo daima imekuwa ikiripoti habari za mazingira na maendeleo ya uchumi kwa ujumla, hasa vijijini, inatambua kwamba mabadiliko ya tabianchi yanaweza kufanya hali ya hewa yote kuwa mbaya, yataongeza ukame katika maeneo kadhaa, kubadili mfumo wa uzalishaji wa wanyama pamoja na kuongeza magonjwa duniani, na kusababisha maeneo ya dunia yaliyo chini kuzama katika bahari ambayo inazidi kupanda juu.
Matokeo ya mabadiliko hayo yatasababisha machafuko ya kisiasa, ukame wa kutisha, njaa, kuharibika kwa mfumo wa ikolojia na mabadiliko mengine yatakayoifanya Dunia kuwa mahali pa kutisha na pasipofaa kuishi.
Vimondo!
 Vimondo (Asteroids) ndivyo vinavyochukua sehemu kubwa katika filamu za kutisha hasa zile za kisayansi, lakini wanasayanasi wanahofia kwamba upo uwezekano pia wa jiwe kubwa kutoka angani, yaani kimondo, ambalo linaweza kuporomoka na kuja kuikandamiza na kuifuta kabisa Dunia.
Inawezekana kimondo ndicho kilichowaua wale wanyama wakubwa wa ajabu (dinosaurs) ambao tumeendelea kuwaona kama ni ngano za kufikirika na kusadikika ingawa kweli walikuwepo ulimwenguni.
Na katika tukio la Tunguska, kimondo kikubwa kiliharibu eneo la maili 770 (takriban kilometa 2,000) za msitu wa Siberia mnamo mwaka 1908.
Jambo linaloogofya, pengine, ni ukweli kwamba wanaanga wanafahamu tu kuhusu kuporomoka kwa mawe ya angani ambayo yanaishia kwenye anga za mbali katika mfumo wa jua (solar system).
Magonjwa ya kutisha


Majanga ya magonjwa mapya ya kutisha yanayoua bila tiba wala kinga yanaibuka kila mwaka: Magonjwa yaliyoibuka katika miaka ya karibuni ni pamoja na SARS (severe acute respiratory syndrome), mafua ya ndege, na ugonjwa mpya kabisa wa MERS unaosababishwa na virusi aina ya coronavirus ambao ulianzisha Saudi Arabia. Hii ni mbali ya Ukimwi na Ebola. Na kwa sababu ya maendeleo ya sasa yanayotufanya tuunganike bila shida, uchumi wa dunia, gonjwa la kutisha linaweza kusambaa haraka kama moto wa nyikani.
MaendeleoVijijini inazo kumbukumbu jinsi ugonjwa wa Ebola ulivyomaliza watu wengi hasa Afrika Magharibi na bado unaendelea kuwa tishio duniani mpaka sasa.
"Hofu ya majanga ya magonjwa yanayoweza kuiangamiza dunia mara moja ni kubwa sana," anasema Joseph Miller, mwandishi mwenza (akishirikiana na Ken Miller) wa kitabu cha "Biology" (Prentice Hall, 2010).
Majanga ya kujitakia
Magonjwa ya asili siyo pekee yanayoweza kuleta hofu duniani. Mwaka 2011, jamii ya wanasayansi ilipagawa baada ya kugundua kwamba watafiti walikuwa wametengeneza kirusi kipya cha mafua ya ndege kijulikanacho kama H5N1 ambacho kilikuwa kinasambaa kupitia njia ya hewa.
Matokeo hayo yalizua taharuki duniani baada ya kubaini kwamba magonjwa ya kutisha ambayo ni ya kutengenezwa yangeweza kusambaa kutoka kwenye maabara za utafiti au yangeachiliwa kwa makusudi kabisa, na kusababisha janga la dunia.
Kuvu (Fungus) miongoni mwetu
Japokuwa bakteria ni hatari, lakini majanga ya kuvu (fungus) ni hatari zaidi, anasema David Wake, mhifadhi katika Makumbusho ya Wanyama na Wadudu (Museum of Vertebrate Zoology) katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley.
"Tumekumbana na ugonjwa mpya wa fangasi unaowashambulia wanyama wa jamii ya amfibia ambao una madhara ya kutisha," alisema Wake akizungumzia fangasi wa aina ya chytrid ambao wanaua chura wengine nchini Marekani.
Ni wazi kwamba akitokea fangasi mwingine wa kutisha kwa binadamu yatakuwa ni majanga. Na japokuwa bakteria ni hatari, kuna dawa za kutosha kukabiliana nao. Kwa ulinganisho, hatufahamu sana kuhusu kutibu magonjwa yanayosababishwa na fangasi kuliko ambavyo tunafahamu magonjwa yanayosababishwa na bakteria, alisema Wake.
Vita vya Nyuklia
 
Mataifa mengi hivi sasa yanakusanya malighafi mbalimbali za kutengeneza silaha za maangamizi, hasa za nyuklia. Ingawa mengi kati ya mataifa hayo yamekuwa yakikanusha hadharani katika vikao vya usalama duniani, lakini bado ukweli uko pale pale kwamba yanatengeneza silaha hizo na yamezificha, huku yakiendelea kutafuta malighafi kila pembe ya dunia, hasa madini ya uranium.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo hivi sasa zinachimbwa uranium na kampuni inayochimba inamilikiwa na serikali ya Urusi, ambayo kwa miaka mingi inafahamika kwamba iko imara kijeshi na inaendelea kufanya tafiti za silaha mbalimbali.
Kwa hiyo, wanasayansi wana hofu kubwa kuhusu tishio la mwisho wa dunia: hasa vita ya dunia ya nyuklia. Fikiria kama hivi sasa tu wapo watu wanaovaa mabomu ya kujitoa muhanga na kufanya ugaidi, je, akitokea mwendawazimu mmoja akaamua kuyafurumua mabomu ya nyuklia ili ‘tufe wote’ maana yake ataifuta dunia.
Ukiacha jitihada za silaha kali za Kim Jong Un wa Korea Kaskazini pamoja na silaha za nyuklia za Iran, kuwepo kwa viwanda vingi vya nyuklia duniani kunaweza kuisambaratisha dunia kama silaha hizo zitatua kwenye mikono ya mwendawazimu mmoja.
Kiama kinaweza kufika kutokana na silaha za nyuklia au silaha za kibaolojia au mabadiliko ya tabianchi.
Ujio wa maroboti
Filamu ya "The Terminator" iliyochezwa na Arnold Schwarzenegger inaweza kuwa ni ubunifu tu wa kisayansi, lakini mashine na mitambo ya mauaji isiyoendeshwa na watu inaweza kuwa karibu na uhalisia.
Miaka kadhaa iliyopita Umoja wa Mataifa ulipiga marufuku matumizi ya maroboti ya mauaji — inawezekana hiyo ilitokana na ukweli kwamba wataalamu wanahofia kuwa njia nyingi zimekuwa zikiyatengeneza.
Wanasayansi wa kompyuta wanafikiria kuhusu kukaribia kwa ‘umoja’ (singularity), mahali ambapo uwezo wa kufikiri wa kutengeneza, yaani artificial intelligence, utazidi uwezo wa kibinadamu.
Kama maroboti hayo yatakuwa muhimu katika kusaidia au yataharibu uwepo wa binadamu ni suala ambalo linahitaji mjadala. Lakini mambo mengi yatakwenda kombo ikiwa yatakuwepo maroboti yenye uwezo mkubwa kuliko binadamu yakiwa yametengenezwa kama silaha za mauaji ambayo yataiongoza dunia.
Ongezeko la watu
Hofu ya ongezeko kubwa la watu duniani limeonekana kuanzia karne ya 18, wakati Thomas Malthus alipotabiri kwamba kuongeza kwa watu kutasababisha njaa na kuijaza dunia.
Huku idadi ya watu duniani ikiwa bilioni 7 na ikiendelea kupanda kwa kasi ya ajabu, wahifadhi wengi wanadhani kwamba ongezeko la watu ni mojawapo ya majanga ya dunia.
Ni wazi, kwamba siyo kila mtu anakubaliana: Wengi wanadhani ongezeko la watu linaweza kutengemaa katika miaka 50 ijayo, na kwamba wanadamu watarekebisha madhara yake yanayotokana na wingi wa watu kwa sasa.
Madhara ya barafu
Pamoja ma matukio haya kwamba yatatokea, wanasayanasi wengi wanadhani kwamba madhara ya mabonge ya barafu yanaweza kutokea, anasema Miller.
Kwa mfano, ongezeko la joto litaongeza athari za mazingira. Wakati huo huo, mfumo wa ikolojia utaporomoka na kufanya iwe vigumu kuzalisha chakula, huku nyuki wakiwa wametoweka kabisa duniani kutokana na kutokuwepo kwa miti kwani ndio pekee wanaoweza kuchavusha mazao.
Kwa hiyo, badala ya madhara madogo, kuna sababu nyingine ndogo ndogo ambazo zinaweza kuathiri maisha ndani ya Dunia mpaka pale wanadamu watakapotambua hatari hiyo na kuibadilisha, kwa kurejesha hali ya misitu na mazingira kwa ujumla.
 
 
 
chanzo: http://maendeleovijijini.blogspot.com
http://3.bp.blogspot.com/-e0QpO-QtZzE/U5DWDUZasXI/AAAAAAAABWg/QlFF97gwNdc/s1600/RAHA+GIF.gif
GIVE YOUR OPINIONS HERE

0 comments: