Askari akamatwa kwa kudhalilisha maiti
Afisa mmoja wa jeshi la Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo ametiwa nguvuni baada ya kuchafua maiti za
wapiganaji wa waasi nchini humo.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa DRC,
Lambert Mende, ameiambia BBC kwamba Luteni Solomo Bangala alizuiliwa
jana Alhamisi na maafisa wa kijeshi baada ya mapigano kuzuka kati ya
jeshi na waasi wa M23 katika eneo la mashariki karibu na mji wa Goma.Kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa kinatathmini upya hatua yake ya kuunga mkono vikosi vya serikali ya DRC kufuatia shutuma hizo.
Mwandishi wa BBC Maud Jullien aliyepo katika mji wa Goma anasema uwanja wa mapigano ulikuwa takriban kilomita 7 katika vilima kutoka mji huo.
Hapajakuwa na mapigano yoyote katika kipindi cha siku mbili zilizopita na jeshi limesema limefanikiwa kuwafukuza waasi yapata kilomita 6, anasema mwandishi wetu.
Mwezi Novemba, wanamgambo wa M23 waliuteka kwa kipindi kifupi mji wa Goma, kisha wakaondoka baada ya kutimizia msururu wa ahadi ikiwemo kuanzisha mazungumzo na serikali.
Waasi wa M23, ambao kwa wingi wanatoka kabila la Watutsi walijiondoa katika jeshi la serikali mwezi Aprili mwaka 2012, na kuanzisha mapigano yaliyowaacha takrikaban watu 800,000 bila makao katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Mazungumzo ya amani yaliyofanyika nchini Uganda mwaka huu ili kushughulikia malalamishi ya waasi hao yamekwama.
chanzo:bbcswahili
0 comments: