HALI YA SERIKALI KIFEDHA NI TETE
Dar
es Salaam. Miradi mbalimbali ya mashirika ya umma, nchini iliyopangwa
kutekelezwa mwaka wa fedha 2013/14 huenda ikakwama kutokana na uamuzi wa
Serikali kuagiza mashirika yote hayo yatoe asilimia 10 ya mapato yake
kwa kuichangia Serikali.
Uchunguzi
uliofanywa na Mwananchi Jumamosi umebaini kuwa tayari Serikali, imetuma
waraka kwa mashirika hayo, ambayo hata hivyo baadhi yapo katika hali
mbaya kwa sasa kutokana na kushindwa kuendeleza miradi kadhaa ya
maendeleo.
Mbali
na mashirika ya umma kutakiwa kuchangia fedha kwenye mfuko wa Serikali,
Serikali pia haijapeleka fedha za ruzuku katika halmashauri mbalimbali
nchini pamoja na kushindwa kuwalipa posho wafanyakazi wake maeneo
mbalimbali.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya halmashauri kushindwa kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyomo kwenye bajeti.
Mtendaji
wa moja ya halmashauri mkoani Pwani aliliambia gazeti hili; “Kwa sasa
kweli hali ni mbaya, hakuna fedha iliyofika kutoka serikalini, hakuna
shughuli inayohitaji fedha ambayo inafanyika.”
Taarifa
za ndani kutoka Wizara ya Fedha zinasema kwamba Serikali haina fedha
kwa sasa ambapo sasa inalazimika kukusanya fedha kutoka katika mashirika
yake ili kuendesha shughuli zake.
Miongoni
mwa mashirika ya umma yanayoguswa na uamuzi huo wa Serikali ni mifuko
ya hifadhi ya jamii ikiwamo NSSF, PSPF, Mamlaka Udhibiti wa Nishati na
Maji(Ewura)Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), Mamlaka ya Hifadhi za
Taifa(Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro(NCAA), Shirika la
Viwango Tanzania (TBS) na mengine kadhaa.
Wakizungumza
na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyakazi wa Idara za
Fedha za mashirika hayo, walieleza kuwa kutokana uamuzi huo wa Serikali
sasa wanalazimika kukaa ili kuandaa upya bajeti za mashirika hayo.
“Ukweli
haya maagizo yana athiri kubwa kwetu kwani tayari tulikuwa tumepanga
bajeti kutokana na mapato na kwa uamuzi huu ambao kimsingi hakuna
mamlaka ya kuyapinga, itabidi tutoe, ila adhari zitakuwepo,”alisema
ofisa mmoja wa juu wa moja ya mashirika ya umma.
Hata
hivyo, alisema kuwa iwapo wangeshauriwa mapema basi walau wangetakiwa
kuchangia asilimia tano kwa mwaka huu wa fedha na mwaka ujao ndipo
ingeongezeka kufikia asilimia 10.
Ofisa
mwingine wa shirika la umma aliyeomba kutotajwa jina alieleza kuwa
uchangiaji huo, ulipaswa kutazama mashirika, kwani yapo yanayojiendesha
kwa hasara, mengine yanapokea ruzuku na mengine yanajiendesha kwa fedha
zake.
Uchunguzi
wa Mwananchi Jumamosi umebaini kwa Tanapa pekee inatakiwa kulipa Sh24
bilioni, zinazotakiwa kukatwa kutoka kwenye bajeti yao ya kutekeleza
miradi ya maendeleo ya shirika na jamii inayowazunguka.
MWANANCHI
0 comments: