Zitto Kabwe Afanya Uzinduzi wa Chama Chake Kipya Cha ACT wazalendo HOTUBA YAKE HII HAPA
Nawashukuru kwa kuwa pamoja nasi siku hii ya kihistoria.
Karibu
Miaka 54 iliyopita tulipopata uhuru, Muasisi na Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 39, mwenye
matumaini makubwa na taifa jipya na alikuwa na ndoto!
Ndoto
yake ilikuwa imejikita katika kuhakikisha taifa letu litakuwa taifa
lisilo na umaskini, dhiki, ufukara; taifa lisilo na tofauti kubwa kati
ya maskini na tajiri; taifa lenye usawa, haki na maendeleo, ambapo
watoto wote wanasoma shule bila kujali kipato cha mzazi; taifa ambalo
wananchi wake wanamiliki uchumi wao.
Ndoto
hii aliiamini kwa dhati na wananchi wote walikubali na kuota nae ndoto
hii. Alilisimamia kwa maneno na vitendo kupitia Azimio la Arusha, sera
zake na uongozi wake wa kizalendo. Mpaka mauti ilipomkuta aliamini
katika misingi hii aliyojitahidi kuturithisha. Lakini miaka 16 baada ya
kifo chake, ndoto yake imeyeyuka!
Tulilonalo ni jinamizi alilolihofu Nyerere.
Leo hii:
- Watanzania wachache wameondoka katika unyonge na dhiki.
- Watanzania wengi bado wapo katika hali ya dhiki.
- Watanzania wachache wameshikilia uchumi: Warasimu, Wanasiasa na Matajiri wachache wenye mitaji.
- Watanzania wengi bado kama Mwalimu Nyerere alivyosema “wananyonywa kiasi cha kutosha; wanapuuzwa kiasi cha kutosha”.
Ndoto ya Mwalimu Nyerere bado haijawafikia wananchi.
- Sasa ndio wakati wa mabadiliko ya kimapinduzi.
- Sasa ndio wakati wa kujenga Uchumi shirikishi ambao utaruhusu kila mwananchi kupata fursa ya kuboresha maisha yake;
- Sasa ndio wakati dola imara ipate nafasi ya kusimamia uchumi;
- Sasa ndio wakati kwa wananchi kuwa na uhuru wa kweli wa mawazo, fikra, kushirikiana, kuabudu;
- Sasa ndio wakati wananchi kuwa na nguvu ya kuwawajibisha viongozi wao;
- Sasa ndio wakati wetu watanzania kujirithisha upya nchi yetu!
Huu
ndio wakati wa kubomoa uchumi wa kinyonyaji na kifisadi na kujenga
uchumi wa wananchi. Haya ndio mabadiliko ya kimapinduzi tunayoyataka.
Hii ndiyo ilikuwa ndoto ya Mwalimu Nyerere, na muda umefika wananchi
turejeshe nchi mikononi mwetu!
Haya
yamekuwa mawazo yangu kwa muda mrefu kwa sababu mimi ni zao la ndoto ya
Mwalimu Nyerere. Nililelewa na mama yangu mzazi pekee mwenye ulemavu;
nimeanza kusoma shule ya msingi nikiwa naenda peku. Lakini kutokana na
kufaulu mitihani vizuri, sikuhitaji kuwa tajiri kusoma mpaka chuo kikuu.
Leo
hii kutokana na elimu bora niliyoipata bure, nimesafiri na kufika
katika nchi zaidi ya 70; nikiwa kama kiongozi nimekutana na
kubadilishana mawazo na watu muhimu duniani kama vile wakuu wa nchi. Sio
mimi peke yangu bali tupo maelfu tuliofaidika na mfumo huu.
Lakini
muhimu kupita yote, nimeweza kutumikia wananchi wa Kigoma na watanzania
bungeni kwa miaka 10. Kama hii si ndoto iliyokuja kuwa kweli, ni nini?
Zitto
Zuberi Kabwe angezaliwa mwaka 2000, angekuwa kijana ambaye
hajakamilisha elimu yake, haelewi lugha za kigeni kama kiingereza, hana
ujuzi wowote na kama Mungu angeendelea kuninyima kipaji cha kuimba kama
sasa ningeshindwa hata kutoka kama Diamond na Mwana FA!
Mwalimu
Nyerere asingepigania ndoto yake miaka ya 60 na 70, ningekuwa kama
mamilioni ya vijana leo ambao wanahangaika kutafuta ajira na kipato bila
ujuzi na elimu.
Na
ndiyo maana siku ya leo ni muhimu kwangu. Nina furaha na heshima kubwa
kuwa katika familia yangu mpya ya kisiasa. Familia inayoaamini katika
itikadi, misingi na tunu ninazoziamini.
Nimezungumza
mara kadhaa kuhusu sababu za kujiunga na chama hiki. Chama cha
Wazalendo ACT- Tanzania inaongozwa na misingi ya Uzalendo, Demokarsia,
Uhuru wa fikra na matendo, Utu, Usawa, Uadilifu, Uwazi, Uwajibikaji na
Umoja katika kila kitu. Chama hiki ni cha wananchi si wenyenchi wa sasa
waliojimilikisha taifa. Chama hiki ni cha watanzania wote bila kujali
kabila, dini, jinsia, rangi ya ngozi au hali ya ulemavu!
Tunapojadili
wananchi kujimilikisha upya nchi yetu ni kupitia usimamizi wa sheria
utakaohakikisha kuwa kuna uwazi na uwajibikaji wa viongozi. Uwazi
tunaouamini ni ule utakaohakikisha kila mwananchi anapata taarifa za
fedha zao, mikataba ambayo Serikali inaingia kwa niaba yao na taarifa za
maslahi, mali na madeni ya viongozi wao.
Tunataka
uwazi katika uendeshaji wa Serikali na sisi tutaanza na uwazi katika
uendeshaji wa chama chetu. Tunataka wananchi sio tu wajione kuwa sehemu
ya uendeshaji wa nchi yao, bali pia wawe sehemu ya uendeshaji wa nchi
yao.
Tunataka
uwazi utakaoruhusu uhuru wa mawazo na uhuru wa wananchi kujieleza bila
kuhofu Serikali kuwachukulia hatua kwa kutoa mawazo yao. Ndio maana ACT
Wazalendo tunapinga vikali miswada ya sheria ambayo Serikali ya CCM
imeiwasilisha bungeni katika mkutano unaoendelea.
Miswada
hii kama vile muswada wa Haki ya kupata taarifa, vyombo vya habari na
ule wa makosa ya mtandao, inalenga kuminya na kunyima haki za wananchi
kuwasiliana kwa uhuru na kutoa mawazo yao kama inavyoainishwa katika
katiba ya nchi.
Tunapojadili
wananchi kurejesha taifa mikononi mwao tunazungumzia uwajibikaji.
Ripoti ya Tume ya Marekebisho ya Katiba ilieleza moja ya sababu kubwa ya
kushamiri rushwa, ufisadi na ubadhirifu nchini ni nanukuu ‘kukosekana
kwa mfumo madhubuti wa uwajibikaji’ nchini kwetu.
Sababu
kubwa ya ACT Wazalendo kupinga Katiba inayopendekezwa ni kwamba Katiba
hiyo imechakachua nia hii ya kuweka mfumo wa uwajibikaji. Ndio maana
tunawaambia wananchi waikatae Katiba hiyo kwa nguvu zao zote! Katiba
inayoepndekezwa inastahili kadi nyekundu, tuikatae na kura ya hapana!
Iwapo
wananchi hawawezi kuwawajibisha viongozi kwa matendo yao hatuwezi
kujenga jamii ya watu wanaoheshimiana na kutii sheria za nchi.
Kila
Mtanzania bila ya kujali cheo chake ni lazima awe chini ya sheria.
Uwajibikaji ni lazima uanze na viongozi. Mnajua kuwa katika maisha yangu
ya kisiasa hili ndio limekuwa jukwaa langu.
Kwa
bahati mbaya tunaishi katika kipindi ambacho wanasiasa wengi wamekuwa
wakikumbwa na kashfa mbalimbali za kifisadi na matokeo yake inajengwa
picha kuwa kila mwanasiasa ni fisadi.
Mfumo
wa Uwajibikaji wenye uwazi utasaidia wananchi kutofautisha wanasiasa
wanaosimamia maslahi ya umma na wale wanaosimamia maslahi yao binafsi na
vyama vyao vya siasa.
Mwungwana
ni vitendo; nimewajibisha watu kwenye Buzwagi na mikataba ya madini,
kwenye matumizi mabaya ya fedha za umma na juzi juzi kwenye akaunti ya
Tegeta Escrow. Lakini matukio haya machache hayatoshi kujenga mfumo
madhubuti wa Uwajibikaji.
Ni
lazima kufanya mapinduzi ya mfumo mzima wa uchumi wa nchi yetu na
kujenga mfumo mpya unaohudumia kila Mtanzania na ambao kila Mtanzania
anajivunia kuujenga. Hatuwezi kuwa Taifa linaloshikiliwa na vikundi vya
wafanyabishara wachache na wanasiasa wanaofadhiliwa na wafanyabishara
hao.
ACT
Wazalendo inataka kujenga Taifa ambalo viongozi wake wanawajibika kwa
wananchi. Hii ndio fikra tunayotaka kurejesha. Hizi ndizo siasa
zilizoasisi Taifa letu. Hatuna budi, ni lazima kurudi kwenye misingi na
kuanza upya!
Kwa sababu ACT Wazalendo imejikita kwenye misingi hii, tumelihuisha Azimio la Arusha.
Sio
tu tumeweka miiko ya uongozi lakini pia tumetunga kanuni za kutekeleza
miiko hiyo na kuifanya kuwa sehemu ya Katiba ya chama chetu. Hitaji moja
kubwa la Kanuni zetu za Maadili ni kutaka kila Kiongozi wa ACT
Wazalendo kuweka hadharani Maslahi yake, Mali na Madeni yake.
Katika
chama hiki huo ndio utamaduni wa kisiasa tunaotaka kuujenga. Kutenda
tunachohubiri hata kabla ya kuingia kwenye uongozi wa Dola.
Chama
cha ACT Wazalendo kimeelekeza kikanuni kwamba kila Kiongozi wa chama
lazima atangaze Mali zake na Madeni yake. Kila Kiongozi lazima aweke
wazi maslahi yake ya kibiashara na mengineyo wazi ili kila anapotenda au
kusema jambo wananchi wajue maslahi aliyonayo au la katika suala
husika.
Viongozi
wote wa kitaifa wa ACT Wazalendo wamefanya hivyo na tutaweka saini zetu
mbele yenu kama mashahidi. Naomba Mwanasheria wetu aje hapa tutekeleze
matakwa haya ya kikanuni.
Fomu
hizi zitakuwa kwenye tovuti ya chama ndani ya muda mfupi ujao ili kila
mtanzaina aone. Kila Kiongozi wa Chama ambaye Miiko ya Uongozi inamtaja
anapaswa kuwa amejaza fomu hizi na kuziwasilisha kwa Katibu wa Kamati ya
Uadilifu katika ifikapo tarehe 30 Juni 2015.
Tunapopinga
Viongozi wa Umma kufanya Biashara na Serikali na hivyo kuwa na mgongano
wa kimaslahi na kushamiri kwa ufisadi, hivyo hivyo tunapinga Viongozi
wa Chama chetu kufanya Biashara na Chama. Ni Marufuku Serikali kugeuzwa
kuwa genge la watu wachache wanaopora rasilimali za Umma. Uadilifu
tunaoutaka Serikalini ni lazima uanzie kwetu tunaohubiri.
Tutafanya
haya kwa kubadilisha siasa zetu kuelekea kwenye masuala yanayowahusu
wananchi; Wakulima, Wafanyakazi, Wafanyabiashara ndogo ndogo, Vijana,
Wanawake na Wazee wetu.
Tunataka
kurejesha nchi yetu Tanzania kwa kujenga uchumi wa wote. Tunaporejea
kwenye Azimio, hatusemi tunakwenda kutaifisha kila kitu na Serikali
kuendesha shughuli zote za kiuchumi. Tunaheshimu na kuthamini sekta
binafsi na mchango wake katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo.
Tunamaanisha kuwa ni lazima Dola isimamie uchumi.
Sio
kazi ya Serikali kufanya biashara. Lakini tunamaanisha kuwa ni lazima
kurekebisha baadhi ya makosa yaliyofanyika kwenye ubinafsishaji na
hususan ubinafsishaji holela uliofanyika kwenye sekta ya Kilimo na
kupora ardhi ya wananchi wetu na kuwageuza kuwa manamba kwenye ardhi yao
wenyewe.
Tunataka kutomokeza ukwepaji kodi.
Tanzania
inapoteza 15% ya makusanyo katika forodha kwa sababu ya ukwepaji wa
kodi. Hii ni sawa na tshs 490 bilioni kwa mwaka, fedha ambazo zingeweza
kuchangia wananchi milioni 4 kwenye hifadhi ya Jamii.
Tanzania
inapoteza takribani tshs 2 trilioni kila mwaka kwenye misamaha ya kodi.
Hii ni fedha ambayo ingeweza kujenga reli mpya ya kati ya kisasa kutoka
Dar mpaka Mwanza na Kigoma ndani ya miaka mitatu. Ili kuondoa upotevu
huu ni lazima kupanua wigo wa kodi, kurahisisha kodi, kupunguza baadhi
ya kodi kama ( PAYE) na kutumia teknolojia kuziba mianya ya ukwepaji wa
kodi.
Vile
vile ni muhimu kuimarisha mfumo wetu wa kodi za kimataifa ili kuzuia
utoroshaji mkubwa unaofanywa na makampuni ya kigeni. Ili tujitegemee
kama Taifa ni lazima kukusanya mapato ya ndani ya kutosha. Ili kukusanya
mapato ya ndani ya kutosha ni lazima kuweka mazingira mazuri ya
biashara hasa kwa wafanyabishara ndogo ndogo kwani ndio wazalishaji
wakubwa wa ajira.
Kwa
Vijana, Taifa hili ni lenu. Asilimia 75 ya Watanzania wapo chini ya
miaka 40. Asilimia 65 ya wapiga kura wapo chini ya miaka 40. Nusu ya
Watanzania ni watoto chini ya miaka 18. Kurejesha nchi kwenye misingi ni
wajibu wa kujenga maisha yenu. Haikubaliki Vijana kuwa mzigo kwa wazazi
kwa sababu tu uchumi hauzalishi ajira za kutosha.
ACT
Wazalendo ndio jukwaa lenu la kufanya mapinduzi ya mfumo wa uchumi ili
kujenga uchumi shirikishi unaozalisha ajira. ACT Wazalendo inataka
kuwajengea mfumo wa hifadhi ya jamii ambapo mtakapokuwa Wazee msipate
tabu za pensheni na matibabu wanazopata Wazee wetu hivi sasa. Shiriki
kujijengea Taifa litakalohakikisha maisha yako ya sasa nay a baadae na
ya kizazi kijacho.
Kwa
Wanawake, Ninyi ndio mhimili wa Taifa hili, wazalishaji wakuu na walezi
wa Taifa letu. Kurejesha nchi kwenye misingi ni wajibu wa kutambua
nafasi yenu stahili katika jamii.
Nikiwa
nimelelewa na Mwanamke mwenye ulemavu na mpiganaji wa kweli wa haki za
wananchi walio pembezoni, sina namna kutoa heshima yangu zaidi ya
kuongoza chama chenye misingi thabiti ya kumkomboa mwanamke. Msitarajie
watu wengine kuwapigania mnapaswa kuchukua hatua kupitia jukwaa hili la
ACT Wazalendo.
Kwa
wafanyabishara, ninyi ndio mnachochea shughuli za Uchumi na kuzalisha
ajira. Kuanzia kwa wamiliki wa maduka madogo mitaani mpaka kwa mameneja
wa maduka makubwa; kutoka kwa wachuuzi na mama lishe mpaka kwa wamiliki
wa viwanda na biashara; mnaamka kila siku asubuhi kujenga Taifa hili kwa
kuzalisha mali na huduma.
Baadhi
yenu ambao mnamiliki viwanda, mashirika makubwa na kutoa ajira kwa
maelfu ya wananchi, mmeanza mkiwa mnashona viatu na sare za shule, au
mkitengeneza na kuuza mkate.
Mmepata
utajiri wenu na mali zenu kwa juhudi na jasho lenu na kutokana na fursa
za kiuchumi zilizokuwepo kipindi hicho ambacho hakikuangalia dini,
kabila, uwezo wa kifedha au rangi ya ngozi.
ACT
Wazalendo inataka kuwawekea mazingira bora ya biashara halali lakini
pia kuhakikisha mnalipa kodi zenu na kutonyonya wafanyakazi wenu.
Tunataka
kuwawekea mfumo rahisi wa kodi, wenye kueleweka na unaowapa motisha
kuzalisha zaidi ili kuongeza ajira zaidi na kupanua Pato la Taifa.
Msipotimiza wajibu wenu biashara zenu hazitashamiri. Kurudi kwenye
misingi ya Taifa hili ni kurejesha maadili katika biashara zenu.
Kwa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi, ninyi ndio mnaolilisha Taifa letu na kuleta fedha nyingi za kigeni kupitia mauzo nje.
Kwa
miongo mitatu sera za nchi zimewaweka pembeni na hivyo uchumi wenu
kusinyaa. Viwanda vyote vya kusindika mazao yenu vimeuzwa kwa bei ya
kutupwa licha ya kwamba jasho lenu ndio lilitumika kuvijenga.
Miundombinu ya barabara, maji, umeme na mawasiliano haiwafikii ili
muweze kupata masoko.
Hamna
hifadhi ya jamii wala bima ya mazao yenu. Ardhi yenu wamepewa
wawekezaji na mnakodishiwa, mnapanga kwenye ardhi yenu wenyewe. Mmeachwa
mkijihangaikia.
Kurejesha
nchi kwenye misingi kutawarudishia heshima yenu katika nchi yetu. ACT
Wazalendo ndio jukwaa sahihi kwenu kuhakikisha kuwa tunajenga uchumi
shirikishi ambao mtafaidika na jasho lenu. Hamna cha kupoteza isipokuwa
minyororo ya kinyonyaji.
Kwa
Watanzania wote mnaonisikiliza leo, katika ukumbi huu na popote mlipo
kupitia vyombo vya habari, mnamo mwaka 1978 Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere alitangaza vita dhidi ya nduli Idi Amini na kusema;
“Tutampiga. Sababu za kumpiga tunazo, nia tunayo, uwezo wa kumpiga tunao”.
Tanzania ipo katika vita hivi sasa.
- Vita dhidi ya Ufisadi,
- vita dhidi ya uporaji wa rasilimali zetu,
- vita dhidi ya Siasa chafu.
- Vita dhidi ya Uchumi wa kinyonyaji.
- Vita dhidi ya kuporomoka kwa Utaifa wetu.
Tunapaswa
kufanya jambo moja tu, nalo ni kupigana vita hizi. Ni vita kwa ajili ya
kurejesha ndoto tuliyoota miaka 54 iliyopita na Muasisi wetu Mwalimu
Julius Nyerere. Tunataka kurejesha nchi kwa wananchi, tunataka
kujimilikisha nchi yetu. Wananchi wawe WENYE nchi!
Tutimize ndoto yetu ya kuona;
Tutimize ndoto yetu ya kuona;
- Tanzania yenye Dola madhubuti,
- Tanzania yenye Wananchi wenye mwamko,
- Tanzania yenye sekta binafsi iliyochangamka,
- Tanzania yenye uchumi unaonufaisha watu wote.
Sababu tunazo, nia tunayo na uwezo tunao. Twendeni tukajenge Chama kitakachorejesha misingi ya Taifa letu.
thanks:eddy blog
0 comments: