Sudan, Sudan Kusini, Somalia, Chad - hayo ndiyo baadhi ya mataifa
ambako watoto wamelazimishwa kupigana vita katika miaka iliyopita. Umoja
wa Mataifa unakadiria kuwa watoto 250,000 wanatumikishwa na jeshi au
waasi katika mapambano ya kivita. Ripoti ya Umoja wa Mataifa
inaorodhesha pande 52 za kivita katika mataifa 23 ambazo zinawatumikisha
vibaya watoto.
Kupitia madawa ya kulevya
Kwa bahati mbaya matumizi ya watoto yana faida nyingi kwa makundi ya
silaha, alisema Ninja Charbonneau wa UNICEF katika mahojiano na DW:
"Watoto ni wapiganaji wasio ghali na ambao ni wepesi wa kudanganya. Mara
nyingi hulishwa madawa ya kulevya na kupewa propaganda na kuonyeshwa
filamu za ukatili. Wanaishi katika hofu ya kuuawa ikiwa watakaidi amri
za wakubwa wao.
Msaada kupitia wanajeshi wa kulinda amani wa UN
Wakati mwingine watoto hufanikiwa kutoroka au kukombolewa na
wanajeshi wa serikali. Wanajeshi hawa watoto wanakabidhi silaha zao kwa
vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, na kisha hupatiwa mgao wa
chakula na dawa. Watoto wanajeshi wanakabiliwa hasa na tatizo la
utapiamlo, vidonda vilivyoambukizwa, magonjwa ya zinaa na athari za
madawa ya kulevya na matatizo ya akili.
Kurejea katika maisha ya kawaida
Watoto hukabiliwa na ugumu katika kuanza maisha upya na kusahau
waliyopitia. Miili yao na roho zao zimejaa makovu. Hivyo ni muhimu kwao
kushirikishwa tena katika jamii. Katika makambi, watoto hupelekwa
shuleni hadi familia zao zinapowafuata. Lakini hili linachukuwa muda na
linakuwa gumu pale migogoro ya kivita inapokuwa inaendelea.
Kukabiliana na kumbukumbu
Moja aliefanikiwa kutoka ni China Keitetsi. Kama mwandishi,
anakabiliana na uzoefu wake wa kikatili kama mwanajeshi mtoto wa zamani
nchini Uganda katika kitabu chake "Machozi kati ya mbingu na Dunia".
Anasimulia juu ya miaka ya kwanza baada ya kukimbilia nchini Denmark, na
kujaribu kusahau ukatili wa vita na kujifunza kuishi maisha yasiyo na
wasiwasi.
Furaha kamili
Pia Emmanuel Jal alikuwa mwanajeshi mtoto. Hii leo ni nyota wa
kimataifa wa muziki wa Hip Hop. Lakini pia hawezi kusahau uzoefu mbaya
wa vita. Mashairi yake yanahusu vita nchini Sudan. " Kupitia mashairi ya
nyimbo, mtu anaweza kuwasabishia watu kuuawana au kusameheana," anasema
mwanaharakati huyo wa amani kwa sasa.
Siku ya kuwakumbuka watoto wanaotumikishwa vitani
Protokali ya hiari kwa Mkataba wa kimataifa kuhusu haki ya mtoto juu
ya ushirikishwaji watoto katika migogoro ya kivita imeridhiwa na mataifa
150. Protokali hiyo ilianza kutekelezwa mnamo Februari 12, 2002. Tangu
wakati huo dunia imekuwa ikiadhimisha siku ya kuwakumbuka watoto
wanaotumikishwa vitani. Siku hiyo inaadhimishwa kila 12 mwezi wa
Februari kukumbuka hatma ya watoto hao.
Ni lini mtoto anakuwa mtoto?
Kulingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto wa mwaka 1989,
kila mshiriki wa vita alie chini ya miaka 15 ni mwanajeshi mtoto. Mwaka
2002 umri wa kuandishwa jeshini ulipandishwa hadi miaka 18. Usaili wa
kujitolea kwa walio zaidi ya miaka 14 ni halali chini ya sheria za
kimataifa. Lakini kwa mashirika ya haki za binaadamu, wapiganaji wote
walio chini ya miaka 18 ni wanajeshi watoto.
Huburutwa kwenye migogoro
Nyumba zilizopigwa kwa mabomu, wanafamilia waliouwawa au marafiki
walliojeruhiwa: Vita huwaathiri zaidi watoto, kama ilivyo hapa katika
mji wa Syria wa Aleppo. Watoto wengi huburuzwa katika mgogoro na
wanalaazimika kupigana, ili kulinda makaazi yao na kuweza kujinusuru
wenyewe.
Katika jina la ugaidi
Kundi la kigaidi la Dola ya Kiislamu IS hutumia vurugu hata dhidi ya
watoto: Kulingana na Umoja wa Mataifa, IS iliwatumia watoto kama
waripuaji wa kujitoa muhanga au ngao za kibinaadamu. Baadhi
wanalaazimishwa hata kuuwa watu. Licha ya vitendo vya kinyama vya IS,
kundi hilo bado linawavutia vijana.
Si tu katika uwanja wa vita
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF,
watoto wadogo huandikishwa jeshini na makundi ya waasi na wanamgambo
wanaoiunga serikali katika migogoro - ikiwa ni pamoja na wavulana na
wasichana. Mayatima ama huuzwa au kutenganishwa na familia zao, kisha
wanalaazimishwa kushiriki mapigano, kushughulikia ugavi au hata
kutumikishwa kingono.
chanzo:dwswahili
0 comments: