Kituo cha Kukusanya Matokeo UKAWA Wavamiwa
Polisi jijini Dar es Salaam jana usiku walivamia kituo cha kukusanya matokeo ya nchi nzima cha Chadema kilichopo Kijitonyama na kuwakamata watu wote wanaokiendesha.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene alisema tukio hilo lilitokea saa nne usiku wakati vijana hao wakiendelea kukusanya matokeo hayo.
Alisema kituo hicho kilichokuwa kikiendeshwa na vijana 800 na wengine maelfu waliokuwa mikoani wakituma matokeo, kilianza kazi hiyo jana asubuhi kikilenga kukusanya matokeo yote, kuyajumlisha na kujua mshindi kabla ya matokeo ya jumla ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Kituo chetu kinafanya kazi ile ile kama inayofanywa na kituo cha CCM kilichopo maeneo ya Mlimani City, tunashangaa polisi kuwakamata watu wetu,” alisema Makene.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema kwa sasa polisi wanafanya operesheni nyingi na watu mbalimbali wanakamatwa, hivyo asingeweza kujua kama watu hao pia wamekamatwa katika operesheni hiyo.
chanzo: http://mchomvunews.blogspot.com
0 comments: