PAPA FRANCIS ALIVYOPOKELEWA NCHINI KENYA AHIMIZA AMANI NA UWAZI
Papa
Francis ameanza ziara yake Afrika kwa kuhimiza umoja, uwazi,
kuwathamini vijana na kuyatunza mazingira. Kiongozi huyo wa Kanisa
Katoliki aliwasili Nairobi mwendo wa saa kumi unusu jioni na
kukaribishwa kwa shangwe na viongozi wa kisiasa na kidini uwanja wa
ndege.
Baada
ya kuwasili, alielekea Ikulu ambako alipanda mti kisha kukutana na Rais
Uhuru Kenyatta kabla ya kutoa hotuba yake ya kwanza.Akimkaribisha kutoa
hotuba, Rais Kenyatta, alieleza umuhimu wa ziara ya kiongozi huyo wa
kidini, akimkumbusha kwamba kesho ni siku ya mapumziko na siku ya
kitaifa ya maombi Kenya.
Aliposimama
kuhutubu, Papa Francis alishukuru sana kwa alivyopokelewa kabla ya
kuanza mara moja kusisitiza kuhusu umuhimu wa umoja na utangamano
Afrika. Pia, alikariri umuhimu wa kuwa na uwazi na usawa akisema ndiyo
njia bora ya kumaliza mizozo.
Kadhalika,
alisisitiza nafasi muhimu ya vijana kwa taifa. "Taifa lenu pia lina
vijana wengi. Siki hizi nitakazokuwa hapa, nasubiri sana kukutana na
wengi wao, kuzungumza nao na kuwapa matumaini katika ndoto zao za siku
za usoni.” Alisema.
"Vijana
ndio rasilimali yenye thamani zaidi kwa taifa. Kuwalinda, kuwekeza
katika vijana, na kuwasaidia, ndiyo njia bora zaidi ya kuhakikisha siku
njema za usoni zenye kufuata busara na maadili ya kiroho ya wazee wetu,
maadili ambayo ndiyo nguzo ya jamii.”
Moja
ya masuala ambayo amekuwa akitilia mkazo ni kutunza mazingira. "Kenya
imebarikiwa sio tu na umaridadi, katika milima, mito na maziwa, misitu,
nyika na maeneo kame, bali pia katika utajiri wa maliasili,” alisema.
"Tuna
wajibu wa kupitisha maumbile haya yakiwa hayajaharibiwa kwa vizazi
vijavyo. Maadili haya yamekuwepo kwenye jamii za Kiafrika.”
Kadhalika,
alisitiza umuhimu wa usawa katika jamii na kuwajali wanyonge. Papa
alitumia Kiswahili kuhitimisha hotuba yake, akisema: "Mungu abariki
Kenya!”
Alikuwa
ameandika maneno yayo hayo kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa
Twitter alipokuwa safarini, saa moja hivi kabla ya kuwasili Kenya.
Leo, Papa Francis amepangiwa kuongoza ibada ya misa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Nairobi.
Ataondoka Kenya Ijumaa kuelekea Uganda. Atakamilisha ziara yake Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Taarifa na BBC Swahili na Picha na Ukurasa wa Rais Wa Kenya
0 comments: