Ndege ya Iran yapiga picha manowari ya Marekani

...................


 Picha

 Picha zilizotolewa na shirika la Irin zinaonyesha manowari ya kuchukulia ndege za kivita 
 
Ndege ya Iran isiyokuwa na rubani ilipaa juu ya manowari ya kutumiwa na ndege za kivita za Marekani na kupiga picha wakati wa mazoezi Ghuba ya Uajemi, shirika la habari la serikali ya Iran limetangaza.
Picha zinazodaiwa kuonyesha manowari ya Marekani ambayo jina lake halikutajwa, imeonyeshwa kwenye runinga na shirika hilo.
Kamanda wa jeshi la wanamaji la Iran amesifu operesheni hiyo kwa kukaribia sana manowari hiyo “na kupata picha za ufasaha kuhusu majeshi ya taifa la kigeni”.
Marekani imesema ndege isiyo na rubani ya Iran ilipaa juu ya moja ya manowari zake, lakini haikusema iwapo kisa hicho ndicho kilichoangaziwa na Iran.
Ndege hiyo haikutoa hatari yoyote kwa USS Harry S Truman, lakini hatua hiyo “haikuwa ya kawaida na haikuwa ya kitaalamu”, shirika la habari la Reuters limemnukuu msemaji wa jeshi la wanamaji la Marekani.
Bi Nicole Schwegman amesema kisa hicho kilitokea tarehe 12 Januari, ambayo ndiyo siku Iran iliwazuilia kwa muda mabaharia 10 wa Marekani waliokuwa wameingia maeneo ya bahari ya Iran kimakosa.
Ripoti ya shitika la habari la Iran, Irinn, haukusema ni lini ndege hiyo ilipiga picha hizo ila tu ilitaja kwamba ilikuwa siku ya tatu ya mazoezi ya jeshi la wanamaji.
Shirika la habari la AP linasema hii inaonyesha huenda kisa hicho kilitokea Ijumaa, kwani jeshi la wanamaji la Iran lilianza mazoezi mapema wiki hii.
  Iran
Nyambizi ya Iran pia inadaiwa kushiriki operesheni hiyo
Nyambizi ya Iran pia ilishiriki katika operesheni hiyo ya kufuatilia shughuli za maadui, shirika la habari la Iran lilisema.
Mkuu wa majeshi ya wanamaji ya Iran Habibollah Sayyari, ameambia runinga ya taifa kwamba hiyo ni ishara ya “ujasiri, uzoefu na uwezo wa kisayansi wa wataalamu wetu wa ndege zisizo na marubani”.
Iran iliondolewa vikwazo ilivyowekewa kutokana na mpango wake wa nyuklia mapema mwezi huu, na kuimarisha uhusiano wake na nchi za Magharibi.
Lakini siku chache baadaye, Marekani iliweka vikwazo kuhusiana na mradi wa makombora ya masafa marefu wa Iran.
Iran ilisema vikwazo hivyo, vinavyoathiri idara 11 na watu binafsi wanaohusika na mpango huo ambao hawataruhusiwa kutumia mfumo wa benki wa Marekani, “havina msingi wowote kisheria na kimaadili”.

chanzo:bbcswahili
http://3.bp.blogspot.com/-e0QpO-QtZzE/U5DWDUZasXI/AAAAAAAABWg/QlFF97gwNdc/s1600/RAHA+GIF.gif
GIVE YOUR OPINIONS HERE

0 comments: