HIVI TZ NI UWANJA WA KUJALIBIA MABOMU?:MNYIKA AKOSWA NA BOMU
Picha na Maktaba yetu
Mbunge wa
Ubungo, John Mnyika alinusurika kupigwa na bomu la machozi lililorushwa na
polisi waliokuwa wakizuia kufanyika mkutano ulioitishwa na chama cha Demokrasia
na Maendeleo CHADEMA jana.
Tukio hilo
lilitokea katika eneo la Mabibo kwenye viwanja vya Sahara ambapo bomu hilo
lilimpata mtu aliyekuwa karibu na Mnyika anayeitwa Thomas Jerome, aliyejeruhiwa sehemu ya paja.
lilimpata mtu aliyekuwa karibu na Mnyika anayeitwa Thomas Jerome, aliyejeruhiwa sehemu ya paja.
Baada ya
kurushwa kwa bomu hilo, polisi walitaka kumchukua majeruhi huyo ili wamweke
kwenye gari lao apelekwe hospitalini, lakini Mnyika aliwaelekeza wafuasi wa
CHADEMA kumchukua kwa madai kitendo kilichofanywa na askari hao kililenga
kuficha ushahidi wa jambo hilo.
Polisi
waliokuwemo eneo la tukio waliamua kukubaliana na matakwa ya wafuasi wa CHADEMA
waliomchukua Jerome na kumpeleka hospitali ambako hali yake inadaiwa inaendelea
vizuri.
Akielezea hali
ilivyokuwa akiwa katika mkutano mwingine uliofanyika Ubungo, Mnyika alisema
polisi walifika katika viwanja vya Sahara wakiwa na magari matatu kwa lengo la
kutawanya wafuasi wa CHADEMA wasifanye mkutano wakidai haukuwa na baraka za
jeshi hilo.
Mnyika alisema
polisi hao walisema sababu ya kuuzuia mkutano huo ni uwepo wa ziara ya Makamu wa
Rais katika Wilaya ya Kinondoni, hivyo walikuwa wameelekeza nguvu zao katika
ziara hiyo, kwamba hawakuwa na uwezo wa kuulinda mkutano wa
CHADEMA.
“Nikiwa
nimejiandaa kupanda jukwaani ndiyo polisi walikuja kusema tuache tusifanye
mkutano, nilisogea karibu na gari kumlalamikia ofisa wa polisi kwani kitendo cha
kuahirisha mkutano kwa barua waliyoileta saa sita mchana siku ya mkutano wakati
sisi tuliwapa taarifa siku nne zilizopita ilikuwa sio haki.
“Nilimwambia
ofisa huyo wa polisi kuwa nilikuwa najadiliana kwa simu na viongozi wakuu wa
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Inspekta Jenerali wa Polisi
Said Mwema kumlaumu kutumika vibaya kwa Jeshi la Polisi.
“Nilipokuwa
bado najibizana naye bila fujo zozote, bomu lilirushwa kutoka ndani ya gari ya
polisi na kupita karibu na mimi likamjeruhi mtu aliyekuwa karibu yangu, ki
ukweli nimeshangazwa sana na matumizi mabaya ya silaha za moto,”
alisema.
Aliongeza kuwa
katika purukushani zilizotokea baada ya bomu kupigwa, alipoteza nyaraka
mbalimbali alizokuwa amebeba kama ushahidi kuwaonyesha wafuasi wa chama hicho
hasa jinsi serikali ya CCM na wabunge wake walivyopitisha kodi ya huduma za
simu, na kodi ya laini za simu.
Slaa
anena
Aidha katika
mkutano huo ambao awali ulitangazwa kuwa ungehutubiwa na Katibu Mkuu wa chama
hicho, Dk. Willibrod Slaa, haukuweza kuhutubiwa naye kwa kile alichosema kuwa
watu wake wa usalama walimwambia mapema hali si salama kwenye mkutano
huo.
“Nilipata
taarifa kutoka vyanzo vyangu kuwa polisi walikuwa na mpango wa kuleta fujo,
hivyo nikaona kwa kuwa wanatuwinda nisingeenda kuhutubia, pengine bomu
lililomkosa Mnyika lilikusudiwa kwangu au kwa mwingine,” alisema Dk. Slaa
alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu baada ya kutoonekana
mkutanoni.
Zuio
la polisi
Jeshi la
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana liliahirisha mkutano huo wa CHADEMA
kabla viongozi hao kupanda jukwaani.
Liliwapelekea
barua ya zuio CHADEMA inayosomeka: “Kumbuka barua ya tarehe 17 Julai, yenye
kumb.
CHADEMA/MKT/UBUN/015/2013 uliyomwandikia Kamishna wa
Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam. Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam amezuia kufanyika kwa mkutano huo tarehe 21 Julai 2013 katika viwanja vya
Sahara, Mabibo kwa sababu siku mliyoomba kufanya mkutano wenu wa hadhara, Wilaya
ya Kinondoni ina mapokezi ya ugeni wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.”
Hata hivyo
Mnyika alipinga sababu hiyo ya polisi kwa madai CHADEMA wamepeleka taarifa kwa
Jeshi la Polisi tangu Julai 17 kwamba wangefanya mkutano katika viwanja hivyo
Julai 21, lakini jeshi hilo halikuwajibu hadi walipokuwa wanaenda
mkutanoni.
CHADEMA wabadili mbinu
Kutokana na
kuzuiwa kufanya mkutano kwenye viwanja vya Sahara, CHADEMA waliamua kuufanyia
Ubungo kutokana na kuomba vibali viwili kwenye maeneo tofauti.
Baada ya
kuzuiliwa Mabibo, kibali cha Ubungo kilikuwa halali, hivyo Mbunge wa Ubungo
aliyekuwa amefika Sahara kwa ajili ya kuhutubia, aliandamana kwa miguu na
wafuasi wa chama hicho hadi Ubungo, huku kukiwa na makachero wengi wa polisi
waliofuatilia maandamano hayo.
Akizungumza na
wananchi katika mkutano uliofanyika Ubungo, Mnyika alisema polisi walifanya
kitendo cha kikatili, kusubiri watu wamalize maandalizi, wakusanyike uwanjani
ndipo wanaleta barua ya kupiga marufuku mkutano kwa kisingizio kuwa katika
Wilaya ya Kinondoni kulikuwa na ziara ya makamu wa Rais katika Jimbo la Kawe na
Kindondoni.
“Sisi tupo
Ubungo, Makamu wa Rais yupo Kawe na Kinondoni, sasa suala la kuzuia mikutano
isifanyike lilikuwa na maana gani? Kama Jeshi la Polisi walisema hawana askari
wa kutosha kulinda mkutano wetu mbona katika kuutawanya wamekuja na magari
matatu?” alihoji.
Mnyika
alitumia muda mwingi kulilaumu Jeshi la Polisi, kwanza kwa kuahirisha mkutano
muda mfupi kabla ya viongozi kupanda jukwaani, lakini pia kitendo cha kurushwa
bomu mahali ambapo hakukuwepo fujo zozote.
Madudu
zaidi ya CCM
Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe ameendelea kuanika madudu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
safari hii akitoa nyaraka za mikakati ya chama hicho tawala kufundisha vijana
kukabiliana na wapinzani.
Akihutubia
mkutano wa hadhara juzi katika Viwanja vya Mahakama ya Mwanzo, Nguzo Nane, mjini
Shinyanga, Mbowe alisema kuwa ili kujilinda dhidi ya vitendo alivyodai
wanafanyiwa na vijana wa Green Guards - kikosi cha vijana wa CCM, chama chao
kitaendelea na mipango ya kuwapatia vijana wao mafunzo ya
ukakamavu.
Mbowe
alionyesha nyaraka mbili za CCM zinazoonyesha kuwa chama hicho tawala kupitia
wanachama wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) kimekuwa kikitoa mafunzo ya ukakamavu kwa
vijana wake, huku nyaraka moja ikionyesha kuwa moja ya malengo ya mafunzo hayo
ni kukabiliana na upinzani.
“Tunashambuliwa, watu wetu wanapigwa, wanateswa,
wanatekwa na wengine kuuawa, kwa sababu tu wanataka mabadiliko na wanapenda
CHADEMA, majuzi mlisikia Waziri Mkuu Pinda anasema wamechoka...sasa tunasema
Pinda kama umechoka ondoka upishe ofisi ya umma hiyo, upishe kwenye ofisi ya
watu kama umechoka, maana kuchoka huko ni kuchoka kwa CCM. Pisheni ofisi sio za
kwenu hizo, ni za Watanzania.
“Wananchi hapa
mkononi nimeshika nyaraka mbili za CCM, moja ni cheti cha kuhitimu mafunzo na
nyingine hapa juu imeandikwa ‘Sera za Msingi za CCM’, sasa mi sitawasomea,
naomba aje hapa jukwaani mtu yeyote anayejua kusoma, awasomee mjue tunaposema
CCM wamekuwa na kikundi kinachoshambulia, kupiga, kutesa, kuteka na hata kuua
Watanzania wenzao eti tu kwa sababu wanaunga mkono CHADEMA, huwa tunamaanisha
nini,” alisema Mbowe.
Mmoja wa
wananchi aliyehudhuria mkutano huo wa hadhara, ambao ulikuwa ni sehemu ya
shughuli za ukamilishaji wa kuzindua Kanda ya Ziwa Mashariki (mikoa ya
Shinyanga, Simiyu na Mara), alipewa kabrasha kubwa na kusoma sehemu
inayozungumzia majukumu ya jumuiya za chama hicho.
Mtandao huu
pia ulifanikiwa kuona kabrasha hilo kwa karibu, ambapo kifungu cha 9.1
kinachozungumzia UVCCM, kinasomeka hivi;
“(i) Umoja wa
vijana wa CCM unapaswa kuwajenga vijana katika itikadi, ukakamavu na mafunzo
yatakayowafanya wajiamini, wawe vijana wenye ari ya kutimiza wajibu wao wakiwa
walinzi wa chama, viongozi na wagombea wa CCM.
“(i) Utaratibu
wa kuandaa makambi ya vijana usimamiwe kwa dhati. Chama kiwe na mipango mizuri
ya kutafuta na kuwateua wakufunzi watakaofaa kuwapatia vijana mwelekeo
unaotakiwa ikiwa ni pamoja na elimu ya uchaguzi/uraia. Mafunzo ya makambi ya
vijana, mbali ya kujifunza nyimbo za hamasa yatilie mkazo pia mafunzo ya
ukakamavu kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya kihuni vya baadhi ya vijana wa
vyama vya upinzani.”
Mbowe pia
aliwaonyesha wananchi waliofurika kwenye mkutano huo cheti cha mmoja wa watu
waliohitimu mafunzo ya makambi ya vijana wa CCM ambacho kilionyesha mhusika
alianza mafunzo Juni 27, 2009 na kumaliza Julai 4, 2009, mkoani
Dodoma.
Cheti hicho
kimesainiwa na watu wawili, mmoja mwenye jina la Jumanne Kitundu, akiwa na
nafasi ya Katibu wa UVCCM, Dodoma mjini na mwingine, Robert Mwinje, Mwenyekiti
wa jumuiya hiyo, Wilaya ya Dodoma mjini.
Cheti hicho
kinaonyesha mhusika (jina linahifadhiwa) alihitimu mafunzo ya masomo ya kanuni
ya umoja wa vijana, wajibu wa vijana katika chama, ulinzi na usalama,
ujasiriamali, ukakamavu, wajibu wa vijana katika uchaguzi, rushwa, ukimwi,
historia ya TANU na ASP pamoja na maadili.
Msimamo wa CHADEMA
Mbowe
alisitiza kuwa CHADEMA kitasimamia azimio la kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho
juu ya kuimarisha kitengo chake cha ulinzi na usalama ikiwemo kuanzisha makambi
ya mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wa chama hicho watakaokuwa na jukumu la
kulinda viongozi wao.
Ingawa msimamo
huo umekuwa ukipingwa na wadau mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi, Msajili wa
Vyama vya Siasa na CCM, Mbowe amesisitiza kuwa hawatarudi nyuma juu ya mpango
huo utakaoimarisha ulinzi.
Kodi
ya laini za simu
Hoja ya tozo
ya simu imekuwa ajenda kubwa kwenye mikutano iliyofanywa na viongozi mbalimbali
wa CHADEMA.
Mwenyekiti wa
Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), John Heche alisema kama wananchi
wasingeipa ushirikiano CHADEMA na kupinga maovu mbalimbali, CCM ingekuwa
imeshauza nchi na wananchi wake.
Alisema tozo
la laini za simu lilipitishwa wakati wabunge wa CHADEMA walipokwenda Arusha
kushiriki maombolezo na mazishi ya marehemu wa tukio la bomu, hivyo serikali
ikaona ipeleke jambo hilo lililobarikiwa na wabunge wengi wa CCM.
“Maana yake ni
nini? Kodi hii kwanza mwananchi maskini kabisa ambaye amedunduliza na kununua
simu, atakuwa analipa sawa sawa na matajiri wakubwa, yaani wewe hapa utakuwa
unalipa kodi sawa na Reginald Mengi...lakini kama hiyo haitoshi, ukipiga
mahesabu utakuwa unalipa kodi takriban shilingi 12,000 kwa mwaka.
“Serikali hii
ya CCM inayowaletea kodi ya sh 12,000 kwa mwaka ndiyo ililazimika kuondoa na
kufuta kodi ya kichwa, baada ya CHADEMA kuwa imefanya hivyo kwenye halmashauri
zake, kwa kuanza na Hai ambako Mwenyekiti Mbowe alikuwa ni mbunge na Karatu kwa
Dk. Slaa. Sasa walifuta kodi ya manyanyaso ya kichwa kwa maelekezo ya CHADEMA
iliyokuwa sh 3,000 kwa mwaka, ambapo watu walikuwa wanakimbia nyumba na
kujificha maporini, wengine wakaliwa na wanyama, sasa wanataka mlipe kimya
kimya, sh 12,000 kwa mwaka. Ni matokeo ya kushindwa kwa sera za CCM,” alisema
Heche.
Mkutano wa Geita
Wabunge wa
CHADEMA wanaotoka Kanda ya Ziwa na viongozi wa chama hicho nao waliendelea
kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali huku wakilalamikia tozo la laini za
simu pamoja na mapendezo ya rasimu ya katiba mpya yaliyotolewa na CCM hivi
karibuni yakipinga mambo mengi yaliyopendezwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Jana, wabunge
hao wa viongozi walifanya mikutano ya hadhara katika mji wa Kasamwa huko Geita
na Sengerema mkoani Mwanza ambako walisema CCM imekosa sifa ya kuongoza ndiyo
maana maisha ya Watanzania yamezidi kuwa magumu kadiri siku zinavyokwenda
mbele.
Wabunge hao
pamoja na viongozi na makada wa CHADEMA ambao wapo kwenye msafara wa kuimarisha
chama katika kanda hiyo, ni pamoja na Ezekiel Wenje (Mbunge wa Nyamagana),
Profesa Kulikoyela Kahigi (Bukombe), Dk. Anthony Mbasa (Biharamulo Magharibi) na
Conchesta Rwamlaza (Viti Maalumu – Kagera).
Viongozi na
makada wengine ni pamoja na mjumbe wa Baraza Kanda ya Ziwa Magharibi, Anwar
Kashaga, katibu wa CHADEMA Manispaa ya Bukoba, Lenatus Kilongozi pamoja na
Mwenyekiti wa Wilaya ya Biharamulo Magharibi, George Kasaiza.
Akizungumza
kwenye mikutano hiyo, Wenje alisema CHADEMA inatarajia kuunda mabaraza ya
wananchi kuhusu muundo wa serikali tatu, na wanatarajia kukusanya saini za
Watanzania kupinga tozo ya kodi mpya ya laini za simu iliyopitishwa hivi
karibuni bungeni.
Alisema kwa
sasa CCM wametoa mapendekezo ya kutaka kusiwepo uwazi wa mikataba, maadili ya
umma na haki za binadamu kwenye katiba mpya, na inataka Spika wa Bunge lazima
atokane na mbunge, jambo aliloliita ni kuendeleza ukandamizaji kwa
wananchi.
“Wakati
CHADEMA tunataka spika na mawaziri wasitokane na wabunge, CCM wao wamependekeza
viongozi hao watokane na wabunge ili waendelee kuwakandamiza Watanzania. CHADEMA
tunataka nchi iwe na mawaziri saba tu, na siyo 15 wa pendekezo la tume na 64
waliopo sasa.
“Si hilo tu,
ibara ya 22 hadi 23 ya rasimu ya katiba mpya, CCM kwa mapendekezo yao wanataka
haki za binadamu zisiwepo kwenye katiba mpya ijayo, bali ziwepo kwenye sheria
tu. CCM haitaki kuwepo malengo ya taifa kwenye katiba mpya!
“Tutakusanya
saini milioni 10 za wananchi kuhusu mapendekezo ya katiba mpya. Pia tutakusanya
saini milioni tano za wananchi kutaka tozo ya laini za simu ifutwe,” alisema
Wenje huku akisisitiza uundwaji wa serikali tatu; Tanganyika, Zanzibar na
Shirikisho.Mbunge wa Biharamuro Magharibi, Dk. Mbasa, mbunge Conchesta, Katibu
wa CHADEMA Manispaa ya Bukoba, mjumbe wa Baraza Kanda ya Ziwa Magharibi, Anwar
pamoja na mwenyekiti wa chama hicho Biharamulo Magharibi, Kasaiza waliishutumu
serikali kwa kushindwa kuwaondolea umasikini wananchi wake.
Walisema kwa
sasa Watanzania walio wengi wanalazimika kuvaa viatu vya ‘yebo yebo’ kwa sababu
ya umasikini unaotokana na kushindwa kwa Serikali ya CCM kuwatumikia wananchi
wake kwa kuwanufaisha na rasilimali zilizopo hapa nchini.
“Serikali ya
chama tawala imekosa sifa ya kuwaongoza wananchi. Tunahitaji tuungane wote
kuiondoa CCM mwaka 2015. CHADEMA ni mkombozi wa Watanzania na ndiyo maana
wabunge na viongozi wake wanapambana usiku na mchana kutwa kupigania maendeleo
ya wananchi,” alisema Dk. Mbasa.
Lewis Mbonde
0 comments: