MIILI YA AL-SHABAAB 11 WALIOUAWA YAANIKWA HADHARANI LAMU

...................



Na KALUME KAZUNGU 
MAMIA ya wakazi mjini Mpeketoni jana walikusanyika kwenye uwanja wa hospitali ndogo ya Mpeketoni kutazama miili ya wanamgambo 11 wa Al-Shabaab waliouawa na wanajeshi wa ulinzi Kenya (KDF) mnamo Jumapili alfajiri.
 

Miili ya Al-Shabaab
Wakazi wa Mpeketoni kaunti ya Lamu wakitazama miili ya magaidi 11 wa Al-Shabaab waliouawa Jumapili asubuhi Juni 15, 2015. Picha/KALUME KAZUNGU 

Furaha, majonzi na ghadhabu, vyote vilionekana kwenye nyuso za wakazi wengi wa Mpeketoni, wakati wakitazama maiti za magaidi hao walioangamizwa na KDF wakati wakijaribu kuvamia kambi ya kijeshi ya Baure kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.



KDF waliamua kuruhusu umma kuitazama miili hiyo ili kusaidia kutambua baadhi yamajangili hao.

Kufikia Jumatatu jioni, ni maiti tatu pekee zilizotambuliwa uraia wake, akiwemo Mkenya ambaye ni kamanda mkuu wa kikosi cha Al-Shabaab ukanda wa Pwani, Lukeman Osman Akashirwa, manaibu wake wawili, Thomas Evans kwa jina jingine Abdul Hakim, ambaye ni Mwingereza pamoja na Mkenya mwingine aliyekuwa mwanabiashara wa Mombasa, Said Hamasa.



Kwenye kikao na wanahabari mjini Mpeketoni Jumatatu, Kamanda mkuu wa polisi wa utawala wa kaunti ya Lamu, Chrispus Mutali, alisema operesheni bado inaendelezwa kote katika maeneo ya Lamu, ikiwemo Mangai, Ishakani, msitu wa Boni pamoja na kaunti jirani za Garissa na Wajir ili kuwanasa na hata kuwaua majangili zaidi.



“Tuko macho kuona kwamba amani inadumishwa Lamu na maisha ya wananchi watukufu hayahatarishwi. Huku mkitazama maiti hizi, ningeomba wakazi kutusaidia kutambua iwapo mnawafahamu majangili hawa,” akasema Bw Mutali.




Baadhi ya wakazi waliohojiwa na Taifa Leo mjini Mpeketoni muda mfupi baada ya kutazama miili 11 ya wakora hao, walionekana kufurahishwa na hatua ya serikali ya kuruhusu umma kujionea magaidi walioangamizwa.



Bi Jane Kariuki, aliambia Taifa Leo kwamba angalau watapata nafasi ya kulala usingizi mnono baada ya kujionea kazi inayofanywa na walinda usalama.



“Kitambo hatukuwa tunaonyesha maadui wakati wanajeshi wanapowaua. Hili lilipelekea sisi kukosa imani na walinda usalama wetu tukidhani wanatudanganya tu. Tunafurahi kujionea wenyewe maadui wetu wakiwa wameuliwa. Angalau tutapata usingizi na tungeomba kila gaidi anapouliwa aletwe tumuone,” akasema Bi Kariuki.



Kupunguza machungu



Kwa upande wake, Bw Joseph Ndung’u, aliambia Taifa Leo kuwa kuuliwa kwa wahalifu hao 11 na kuwekwa wazi kwa umma kutazama miili yao angalau kumesaidia wakazi mjini humo kupunguza machungu waliyo nayo hasa baada ya watu kuuliwa na Al-shabaab katika uvamizi wa Juni 15 mwaka jana.



“Watu wa Mpeketoni na Lamu kwa jumla bado tuko na machungu ya watu wetu waliouliwa mwaka jana. Tunashukuru kwamba Mungu anatufanyia miujiza. Tarehe 15 Juni mwaka jana tulikuwa tukilia juu ya watu wetu. Mwaka huu Juni 15 waliotekeleza uvamizi huo pia wamewahiwa. Kuuliwa kwa watu hawa ni dhihirisho tosha kwamba maombi yetu yanasikizwa,” akasema Bw Ndung’u.



Tukio hilo linajiri siku moja baada yawakazi wa Mpeketoni na Lamu kwa jumla kuadhimisha mwaka mmoja tangu uamizi wa Al-Shabaab kutekelezwa eneo hilo na kupelekea vifo vya zaidi ya watu 90.
http://3.bp.blogspot.com/-e0QpO-QtZzE/U5DWDUZasXI/AAAAAAAABWg/QlFF97gwNdc/s1600/RAHA+GIF.gif
GIVE YOUR OPINIONS HERE

0 comments: