Mke Mdogo Wa Slaa Aibua Maswali mazito juu ya chadema, Soma Hapa
HATIMAYE mke mdogo wa
Dk. Willibrod Slaa, Josephine Mushumbusi, ameibuka na kujibu baadhi ya
hoja ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake yeye binafsi na kwa mume wake na
zaidi akisema yote yanayosemwa dhidi yao hayako katika fikra zao kwani
kwa sasa baada ya kuachana na siasa wanajipanga kuelekea upande mwingine
wa kuwa wawekezaji.
Akizungumza na MTANZANIA
Jumamosi kwa njia ya simu jana, Mushumbusi aliitaja mipango yao hiyo
kuwa ni pamoja na kujenga shule na hospitali.
Mushumbusi ametoa kauli
hiyo wakati ambapo gharama zinazokadiriwa kufikia shilingi milioni 50
alizozitumia mume wake katika mkutano wake na waandishi wa habari mapema
wiki hii zikizua mjadala mpana wa alikopata fedha hizo zote.
Pamoja na hilo,
Mushumbusi ambaye anatajwa kuwa katikati ya mpango wa kumrubuni mume
wake licha ya kupuuza hoja kama hizo alipoulizwa walikopata fedha za
kutekeleza miradi mikubwa kama hiyo alisema zimetoka kwa watu aliodai
kuwa ni marafiki zao na kiasi kingine ni asilimia 20 ya vipato vyao
ambavyo walikuwa wakiviweka kwa muda mrefu.
AJIBU MAPIGO
Mushumbusi ambaye tangu
Dk. Slaa azungumze na waandishi wa habari Jumanne wiki hii hajawahi
kuzungumza lolote, alianza kujibu yale yaliyozungumzwa na mke mwenzake
ambaye ni mke wa ndoa wa Dk Slaa aitwae Rose Kamili ambaye juzi
alizungumza na vyombo vya habari na kumtupia tuhuma nzito yeye
(Mushumbusi) na mume wake huyo wa zamani.
Rose alikaririwa na
vyombo vya habari akimtuhumu mumewe kuwa ni muongo na anapelekeshwa na
mwanamke anayeishi naye kwa sasa ambaye ni Mushumbusi.
Akijibu shutuma hizo, Mushumbusi alisema yeye ni zaidi ya siasa rahisi zinazoenezwa dhidi yake.
Alimpuuza Rose kwa
kusema kuwa ameamua kuchanganya matatizo binafsi ya familia na
propaganda za kisiasa, hivyo jambo hilo liko mbali na uwezo wa fikra na
mipango yake kwa sasa.
Mushumbusi alisema yeye
si mwanasiasa kwani ana mambo mengi anayoyafanya mbali na siasa hivyo
shutuma alizotoa Rose kwa Dk. Slaa zingefaa pia kama angewaeleza
Watanzania sababu za kuachwa kwake.
“I’m above with that
cheap politics, you know? (Unajua niko juu ya siasa hizo rahisi?), I’m
activist, I can’t deal with them and I have a lot of things to do out of
politics by the way, I’m not a politician as I told you (mimi ni
mwanaharakati, siwezi kushughulika nao na nina mambo mengi ya kufanya
nje ya siasa, hata hivyo mimi sio mwanasiasa kama nilivyokueleza),”
alisema Mushumbusi.
Mushumbusi alifafanua
kuwa hivi sasa yuko mbali na mambo ya siasa na anaangalia mbele
kulisaidia taifa katika nyanja za elimu, afya na uchumi.
Alisema mipango yao kwa sasa ni kujenga shule, hospitali pamoja na kuwasaidia kina mama katika masuala ya ujasiriamali.
Alisema tayari mipango yao hiyo mipya ilikwishapangwa kwa kushirikiana na Dk. Slaa.
Alisema mbali na fedha za marafiki yeye ni mfanyabiashara wa nafaka na kwa muda mrefu pamoja na mumewe wamekuwa wakiweka akiba.
Hata hivyo, wakati
Mushumbusi akisema kuwa anafanya biashara ya nafaka, gazeti moja la kila
siku (Si MTANZANIA) liliwahi kumkariri hivi karibuni akidai kuwa kwa
sasa anafanya biashara ya mkaa.
“Brother I’m not there
as they think, I’m a focused woman (Kaka sipo hapo kama wanavyofikiri,
mimi ni mwanamke makini), nina mambo mengi ya kulifanyia taifa langu,
nashangaa hata hiyo hoja ya kutelekeza watoto, waulizeni hao watoto kama
hawapajui kwangu, huyo kijana wa kiume kila mara anakuja kwangu hata
wadogo zake wanamfahamu vyema, eti wanasema Dk. Slaa kawatelekeza
wanataka awafanyie nini na wakati watoto wote hao ni above eighteen
(zaidi ya miaka 18) na tayari wamezaa kila mmoja, hoja nyingine you must
think big (kufikiri zaidi),” alisema Mushumbusi.
Kuhusishwa na Kinana, Lukuvi
Akijibu madai ya
kutuhumiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, William Lukuvi ili
kumpa maelekezo mumewe juu ya nini afanye baada ya kujiengua Chadema,
Mushumbusi alikana madai hayo kwa kusema kuwa hana mawasiliano yoyote na
watu hao.
“Sina mawasiliano na
Kinana wala Lukuvi kwanza ni watu ambao sijawahi kufikiria hata siku
moja kama nitazungumza nao, kwanza simpendi huyo Kinana,” alisema
Mushumbusi.
Dk. Mwakyembe na Dk. Slaa
Kuhusu kukutana na Dk.
Mwakyembe katika moja ya vyumba vya Hoteli ya Serena akiwa yeye na mume
wake, Mushumbusi alikana taarifa hizo.
Hata hivyo, MTANZANIA
Jumamosi linafahamu kuwa Mushumbusi alikuwepo katika moja ya vyumba vya
hoteli hiyo ambavyo mume wake alivitumia kukutana na Mwakyembe saa
chache kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.
Pamoja na ukweli huo,
Mushumbusi alisema hana mawasiliano na Mwakyembe ingawa alikiri mume
wake kukutana naye ili kupata ufafanuzi wa baadhi ya hoja za sakata la
Richmond.
“Dk alihitaji kupata
ufafanuzi fulani wa hoja za Richmond, kumbuka ripoti ya Richmond
iliandikwa kisheria zaidi hivyo alimuhitaji Dk. Mwakyembe kwa ajili ya
kupewa ufafanuzi wa baadhi ya vipengele ndipo walipokutana saa chache
kabla ya mkutano na wanahabari,” alisemachanzo:magicnewstz.blogspot.com
0 comments: