HILI LA MADAKTARI KENYA LIFIKIRIWE

...................

Madaktari Kenya wakataa nyongeza ya asilimia 40 iliyopendekezwa na Serikali

mediaPicha ikionesha manesi na madaktari wakiwa kwenye mgomo wao kushinikiza Serikali kutekeleza madai yao ya mshahara.REUTERS/Thomas Mukoya
Chama cha madaktari nchini Kenya kimekataa pendekezo lililotolewa na ikulu ya Mombasa kufuatia mkutano wao na rais Uhuru Kenyatta, ambaye alisema Serikali yake iko tayari kuongeza asilimia 40 ya mshahara wa madaktari hao ili wasitishe mgomo.
Hata hivyo kikao kilichoketi Ijumaa ya tarahe 6 jijini Nairobi, katibu mkuu wa chama cha madaktari Ouma Oluga, amewaambia wanahabari kuwa, baada ya kujadiliana wameamua kutokukubali pendekezo la serikali la asilimia 40.
Oluga amesema kuwa pendekezo lililotolewa na rais Kenyatta licha ya kuwa alionesha nia njema ya kutaka kumaliza mgomo unaoendelea, lakini wao hawako tayari kukubaliana na pendekezo hilo na kwamba mgomo wao utaendelea hadi pale Serikali itakapokubali kutekeleza makubaliano yao ya mwaka 2013.
Mwaka 2013, chama cha madaktari na Serikali ya Kenya walitiliana saini makubaliano ya nyongeza ya mshahara ya asilimia 300 kwa madaktari hao, pamoja na kulipwa marupurupu mengine wanayoidai Serikali.
Mmoja wa madaktari ambao wanashiriki mgomo, wakiandamana hivi karibuni jijini Nairobi.REUTERS/Thomas Mukoya
Mwenyekiti wa chama hicho, Samweli Oroko, amesema kwa sasa wako tayari kuendelea na mazungumzo na Serikali ili kupata muafaka na hatimaye kusitisha mgomo wao, lakini akaongeza kuwa hawako tayari kukubaliana na pendekezo la Serikali ambalo wanasema halitamaliza shida zinazowakabili.
Ni zaidi ya mwezi mmoja sasa, toka madaktari nchini Kenya waanze mgomo wa nchi nzima katika hospitali za uma na binafsi, wakishinikiza Serikali kutekeleza makubaliano yao ya mwaka 2013.
Juma moja lililopita, madaktari nchini humo walimtaka rais kama kiongozi wa juu wa nchi, aingilie kati mgomo wao, ombi ambalo hata hivyo rais Kenyatta alilisikiliza na kukubali kukutana nao mwanzoni mwa juma hili ambapo akapendekeza nyongeza ya asilimia 40.
Mgomo huu wa madaktari umesababisha kuzorota kwa huduma za afya nchini Kenya, ambapo maelfu ya wagonjwa wameendelea kuugulia nyumbani wasijue ni wapi pa kupatia matibabu, huku wengine wakiripotiwa kupoteza maisha

Chanzo:http://sw.rfi.fr/eac/20170106
http://3.bp.blogspot.com/-e0QpO-QtZzE/U5DWDUZasXI/AAAAAAAABWg/QlFF97gwNdc/s1600/RAHA+GIF.gif
GIVE YOUR OPINIONS HERE

0 comments: