UHARAMIA WABADILI UELEKEO AFRIKA.SOMA HAPA

...................

A.Magharibi yapiku Somalia kwa uharamia


Uharamia wapungua Somalia kuliko Kanda ya Afrika Magharibi

Visa vya Uharamia pwani mwa Afrika Magharibi, vimekuwa juu zaidi ikilinganishwa na vile vinavyotokea nchini Somalia. Hii ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa linalohusika na safari za baharini.
Shirika hilo linasema kuwa mabaharia 966 walishambuliwa kanda ya Afrika Magharibi mwaka 2012, ikilinganishwa na visa 851 vilivyorokea pwani ya Somalia.
Maharamia katika kanda hiyo zaidi huiba mafuta na mali ya wasafiri na hata wakati mwingine kutumia mabavu katika kutekeleza wizi.
Watano kati ya mateka 206 waliokamatwa mwaka jana katika kanda hiyo waliuawa.
Ripoti hiyo yenye mada athari za kimaisha kwa uharamia mwaka 2012, ilitolewa na shirika la kimataifa la safari za majini , shirika la Oceans Beyond Piracy pamoja na mashirika mengine.
Yanasema kuwa licha ya kuongezeka kwa visa vya uharamia katika ghuba ya kanda ya Afrika Magharibi nchini Guinea, eneo hilo halijaweza kupewa ulinzi kama pwani ya Somalia.
Maharamia hulenga kushambulia meli zenye kubeba mafuta na kuyauza kwa masoko yasiyo rasmi.
''Nchini Nigeria,pesa hutolewa kwa haraka katika biashara hiyo haramu ikilinganbishwa na Somalia,'' alisema afisaa mmoja anayehusiika na maswala ya usafari wa baharini.
"pia Somalia inaweza kuchukua miezi kadhaa kabla ya kuuza mafuta hayo lakini nchini Nigeria maharamia huchukua mafuta na pesa za wafanyakazi wa meli hizo. Inaweza kuchukua wiki kadhaa tu na waweze kupata pesa kwa haraka. ''
Aidha ripoti hiyo inasema kuwa kukabiliana na uharamia Afrika Magharibi na Somalia inahitaji ushirikiano kati ya juhudi zinazofanywa baharini na zile za ardhini kuweka usalama na kutoa nafasi za ajira kwa watu wanaoweza kufanya kazi ya uharamia.
Wakati huohuo, ripoti inasema kuwa visa vya uharamia vilishuka kwa 78% nchini Somalia mwaka jana ikilinganishwa na visa vilivyoripotiwa mmwaka jana 2011.


Maharamia waiteka meli ya mafuta Nigeria


Meli kubwa ya mafuta

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la wanamaji nchini Nigeria, Jerry Omodara, haijulikani iliko meli hiyo na kwamba juhudi za kuitafuta zinaendelea.
Shirika la kimataifa la mabaharia, liliambia shirika la habari la AFP kwamba mabaharia 23 walikuwa kwenye meli hiyo wakati ilipotekwa na walikuwa wamejifungia ndani ya chumba kimoja salama wakati wa tukio hilo.
Wadadisi wanasema kuwa visa vya uharamia vimekithiri katika maeneo mengi ya Afrika Magharibi.
Shirika la kimataifa la mabaharia, linasema liliweza kurekodi visa kumi na saba vya utekaji nyara wa meli nchini Nigeria, katika miezi ya kwanza sita ya mwaka huu. Linasema kumekuwa na ongezeko kubwa la visa hivyo ikilinganishwa na mwaka 2011.
Mkuu wa kituo cha shirika hilo cha kuripoti visa vya uharamia nchini Malaysia, Noel Choong, amesema kuwa wale waliofanya kitendo hicho, huenda ni kundi moja la maharamia walioteka nyara meli za mafuta nchini Togo mwezi jana, kuiba mafuta na baadaye kuwaachilia mabaharia waliokuwa kwenye meli hiyo.
Luteni Omodara anasema kuwa helikopta moja inatumiwa kuisaka meli hiyo katika juhudi za kuikoa.
Mwaka jana Nigeria na nchi jirani ya Benin zilianza mpango wa pamoja wa kuweka usalama baharani ili kupambana na uharamia.


Kiongozi wa maharamia astaafu Somalia


Haramia nchini Somalia

Kiongozi mmoja wa kijamii nchini Somalia, ameiambia BBC kuwa, mtu mmoja ambaye ametanjwa na Umoja wa Mataifa, kuwa kinara wa utekaji nyara, ametangaza kuwa amestaafu rasmi kutoka kwa uharamia.
Mohamed Abdi Hassan, ambaye anajulikana kwa jina la utani kama "afweyneh" ikiwa na maan mtu mwenye usemi mkubwa nchini Somalia, amewaambia waandishi wa habari kuwa anastafu kutoka kwa biashara hiyo baada ya miaka minane.
Bwana Hassan aliyasema hayo katika kikao kilichofanyika mjini Abado, kati kati mwa Somalia, eneo ambalo maharamia hao wamekuwa wakiwazuilia mateka wao.

Ulinzi umeimarishwa Somalia

Mashambulio ya kiharamia katika pwani ya Somalia, yalipungua kwa kiasi kikubwa mwaka uliopita.
Baadhi ya maharamia waliokamatwa

Wachanganuzi wanasema hali hiyo iliyokana na kuongezeka kwa meli za kijeshi zinazoshika doria katika eneo hilo na pia kujumuishwa kwa walinzi wanaosindikiza meli za mizigo.
Afisa mkuu wa utawala katika eneo hilo amesema kuwa maharamia wengine katika eneo hilo wamekubali kusalimisha silaha zao.
''Tumewashawishi wao kutomiliki silaha na pia kusalimisha zile wanazomiliki ikiwa ni pamoja na mashua na silaha'' Alisema Bwana Mohamed Adan, ambaye ni kiongozi wa Utawala katika eneo hilo la Adado.
'' Wao wamegundua kuwa kwa sasa hawawezi kuendeleza uharamia kama ilivyokuwa hapo awali bila kuzingatia sheria na pia Uharamia kwa sasa haina faida kama ilivyokuwa'' Aliongeza afisa huyo wa utawala.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa

Moja ya meli iliyokuwa imetekwa nyara

Kundi moja la uchunguzi la Mataifa liliripoti mwaka uliopita kuwa Bwana Afweneh, ni mmoja wa watu mashuhuri zaidi kwa mtandao wa uharamia wa Hobyo-Harardhere.
Imeripotiwa kuwa rais mmoja wa zamani wa nchi hiyo alimhaidi hadi ya kibalozi na pia kumkabithi pasi ya kusafiria ya kibalozi ili kuachana na uharamia.
'' Baada ya kushirikia katika vitendo vya uharamia kwa zaidi ya miaka minane, nimeamua leo kuachana nayo na kuanzia hii leo, nitashiriki katika harakati za kupambana makundi ya kiharamia katika pwani ya Somalia'' Shirika la habari la AFP lilimnukuu Bwana Afweyneh.
Kwa mujibu wa shirika hilo la habari, mtandano wake wa uharamia ulihusika na utekaji nyara wa meli ya MV Faina, ya Ukraine mwaka wa 2009, ambayo ilikuwa imebeba magari ya kivita na silaha kutoka urusi.
Meli hiyo iliachiliwa huru baada ya kundi hilo kulipwa kikombozi ya dola milioni tatu nukta mbili, baada ya miezi kadhaa ya majadiliano.



Maharamia kuanza kushtakiwa Mauritious


Maharamia wa Kisomali

Uingereza imetia saini mkataba na Mauritious kuruhusu washukiwa wa uharamia waliokamatwa na jeshi na wanamaji kupelekwa kisiwani humo kwa mashtaka.
Waziri mkuu David Cameron alikutana na mwenzake wa Mauritious Navin Ramgoolam nchini Uingereza kwa makubaliano hayo.
Cameron ameutaja mkataba huo kama hatua muhimu katika vita dhidi ya maharamia sugu wanaoendesha harakati zao katika upembe wa Afrika.
Makubaliano sawa na hayo kati ya nchi hiyo na Tanzania yaliafikiwa katika siku za nyuma.
"Hii ni muhimu sana , mojawapo ya hatua za kufuatilizia mkutano wa London na Istanbul kuhusu Somalia mwaka huu na ni dalili kuwa nchi zingine katika ufuo wa bahari Hindi zinafanya juhudi kubwa dhidi ya uharamia," alisema bwana Cameron.
"uharamia ni kitndo cha uhalifu, na maharamia wanapaswa kufahamu kuwa watakamatwa wakiendesha shughuli zao hata baharini, washtakiwe na kufungwa jela."
Jeshi la wanamaji la Uingereza na majeshi mengine kote duniani yanashika doria katika sehemu ambazo zina shughuli nyingi za meli na ambapo kuna tisho la uharamia.
Mabaharia hukamatwa na kuachiliwa tu wakati kikombozi kikitolewa, na kuwekwa katika mazingira mabaya huku baadhi wakiteswa ili kushinikiza wamiliki wa meli zao kutoa kikombozi.
Uharamia katika pwani ya Somalia, unaaminika kugharimu makampuni ya meli za mizigo takriban dola bilioni 5.6 mwaka jana pekee.


Uharamia wapungua pwani ya Somalia


Meli nyingi sasa zinatekwa nchini Benin na Togo

Idadi ya meli zinazotekwa na maharamia katika pwani ya Somalia, zimepungua sana mwaka huu , kulingana na shirika la kimataifa la safari za majini.
Ni meli sabini pekee zilitekwa nyara katika miezi ya kwanza tisa mwaka huu ikilinganishwa na visa 233 vilivyoripotiwa mwaka 2011.
Juhuzi za kimataifa pamoja na mikakati kipya ya kiusalama ndiyo imekuwa changamoto kubwa kwa maharamia kuendesha kazi zao kulingana na shirika hilo.
Lakini shirika hilo limetoa tahadhari kwa mabaharia kuwa makini wakati wa shughuli zao hasa katika pwani ya Somalia
Mkurugenzi wa shirika hilo, Kapteni Pottengal Mukundan, alisema ni habari njema kusikia kuwa uharamia umepungua, lakini mabaharia hawapaswi kulegea katika kuchukua tahadhari.
Uharamia umeripotiwa zaidi katika Ghuba ya Guinea, ambako jeshi la wanamaji la Nigeria limeanza kushika doria. Pwani mwa Benin na Togo pia ni hatari.
Shirika hilo linasema kuwa visa vya utekaji meli, hupangwa kwa lengo la kuiba mafuta ambayo yanaweza kuuzwa bila wasiwasi katika masoko ya nyumbani.
Ingawa ni kisa kimoja tu kimeripotiwa nchini Somalia katika miezi mitatu iliyopita , maharamia wangali wanazuilia meli kumi na moja wakidai kikombozi huku wafanyakazi 167 wa meli hizo pia wakiwa wamekamatwa.
Wafanyakazi wengine 21 wanazuiliwa katika nchi kavu, wengine sasa wamekuwa wakizuiliwa kwa zaidi ya miezi thelathini.

chanzo:bbcswahili

http://3.bp.blogspot.com/-e0QpO-QtZzE/U5DWDUZasXI/AAAAAAAABWg/QlFF97gwNdc/s1600/RAHA+GIF.gif
GIVE YOUR OPINIONS HERE

0 comments: