Sababu 10 kwa nini John Magufuli atashinda uchaguzi Mkuu wa Urais 2015
1. Tanzania bara na visiwani yako
majimbo ya uchaguzi 266, CCM imesimamisha wagombea Ubunge katika majimbo yote
266 huku Chadema na washirika wake wa Ukawa wakiwa wamesimamisha wagombea
katika majimbo 211 (138 toka Chadema). Kati ya majimbo hayo 266, CCM tayari
imepita bila kupingwa majimbo 7. Ukichukua majimbo 259 yaliyobaki na kutoa 211
ambayo Chadema na washirika wake wamesimamisha wagombea unabaki na majimbo 48
ambayo CCM haina upinzani wa Chadema wala washirika wake wa Ukawa. Majimbo haya
48 CCM ina uhakika wa kushinda walau kwa asilimia 90, ushindi huu si kwa
Wabunge tu bali pia kwa mgombea Urais wa CCM.
2. Watanzania waliojiandikisha
kupiga kura mwaka 2015 ni milioni 24.2. Takwimu zinaonyesha CCM ina wanachama
hai wapatao milioni 8 wenye kadi na wanaolipia ada zao za uanachama kila mwaka.
Kuondoka kwa Edward Lowassa katika Chama Cha Mapinduzi kunamaanisha Magufuli
hatapata kura zote milioni 8 za wana CCM na pia kihesabu si rahisi wana CCM
wote milioni 8 kujitokeza siku ya kupiga kura. Utafiti unaonyesha kwamba wana
CCM watakaopiga kura hawatazidi asilimia 90 ya wanachama wake (milioni 7.2)
huku milioni 7 kati yao wakimpigia kura John Magufuli. Historia ya CCM
inaonyesha ni wanachama wachache sana humpigia kura kada mwenzao anapohama
kugombea nafasi kwa chama kingine, hasa nafasi ya Urais (Rejea: Uchaguzi wa
Urais 1995, mgawanyo wa kura za Augustine Lyatonga Mrema)
3. Mizunguko ya kampeni huzaa kura
za ziada mbali na zile za wanachama. Tayari inaonyesha kwamba Magufuli anapita
karibu kila kata ya Tanzania akitumia barabara huku upande wa Lowassa na
shirikisho la Ukawa hali ikiwa tofauti, ambako amekuwa akifika sehemu chache
akitumia usafiri wa ndege na helkopta na ni wazi hana stamina ya kuzunguka kwa
gari nchi nzima kutokana na tatizo la kiafya. CCM ina mizizi kwenye mashina
kuanzia ngazi ya nyumba kumi. Mtandao huu wa Chama pamoja na safari za mgombea
wao kila kata ni kiashiria kwamba atafikia wapiga kura wengi zaidi hasa sehemu
za vijijini na ambazo si rahisi kufikika. Tafiti zinaonyesha huko ndiko kwenye
wapiga kura wengi na kuwafikia ni hatua moja kuelekea kuzipata kura zao na
kushinda.
4. Chaguzi za Serikali za Mitaa
mwaka 2014 zinaonyesha kwamba CCM ilishinda kwa zaidi ya asilimia 80 kwenye nafasi
za uongozi za serikali za vijiji na mitaa. Ikumbukwe kwamba CCM ilipata ushindi
huu licha ya ushindani mkubwa uliokolezwa na sakata la Escrow wakati huo. Hii
inaonyesha kwamba CCM iliweza kushinda hata wakati huo wa changamoto. Ni mwaka
mmoja tu umepita tangu chaguzi hizo zifanyike. Kitafiti, hiki ni kiashiria
kikubwa kwamba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, CCM kama chama kinaenda
kwenye sanduku la wapiga kura kikiwa na rekodi nzuri kuweza kushinda.
5. Rekodi ya Utendaji ya Magufuli
inavutia Watanzania wengi. Utafiti unaonyesha kwamba wapinzani wake majukwaani
mpaka sasa wanapata wakati mgumu kutaja jina lake moja kwa moja kumuhusisha na
utendaji wa hovyo. Mitandaoni zipo video na nukuu nyingi zikiwemo za Mgombea wa
Ukawa Edward Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wengineo wakisifia
utendaji wa Magufuli. Katika siasa na kampeni, hatua moja kuonyesha mgombea
anashinda ni kushindwa kwa wapinzani wake kumnyooshea kidole moja kwa moja au
kukosa mabaya ya kusema dhidi yake. Asiye na la kukusema vibaya anawapa
wananchi nafasi ya kuona mazuri yako na kushinda.
6. Suala la afya ya wagombea
limekuwa gumzo kubwa katika uchaguzi wa mwaka huu. Huku ikiwa wazi kwamba
Mgombea wa Ukawa Edward Lowassa anaugua ugonjwa wa Parkinson’s kwa muda mrefu
sasa, Magufuli hajawa na changamoto ya afya. Ugonjwa wa Parkinson’s alio nao
Edward Lowassa unaathiri ubongo wa kati, moyo, mishipa ya fahamu na uwezo wa
kufikiri (Afya ya mwili maeneo hayo ni muhimu kiongozi kuwa nayo). Kwa muda
mrefu Lowassa amekuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa huu katika hospitali
maarufu ya Franziskus-Krankenhus mtaa wa Budapester jijini Berlin, Ujerumani.
Kiumri Magufuli ana miaka 55 huku Lowassa akiwa na miaka 63. Wapiga kura
huchagua kiongozi kwa kutazama muonekano na ni wazi kabisa kwamba kwa muonekano
na hali ya kiafya ya Lowassa ni dhoofu na inazidi kudorora siku hadi siku na
kuwakatisha tamaa hata wanaomuunga mkono. Tangu kampeni zianze hakuna mahala
ambapo amewahi kuzungumza kwa zaidi ya dakika 15. Hivyo basi, kwa kadiri siku
zinavyoenda Watanzania watazidi kubaini kwamba Lowassa hana afya ya kuhimili
vishindo vya kampeni wala uwezo wa kumudu majukumu ya Urais.
7. Nguvu ya vyama, oganaizesheni na
ilani. Magufuli anatokea CCM ambayo kama nilivyoeleza juu ina nguvu ya kuwepo
kila kijiji na kila nyumba kumi Tanzania; imetoa marais waliotangulia, na hata
wapinzani wametoka katika CCM hiyo hiyo baada ya kukosa nafasi za kugombea
kupitia chama hicho. Kwa miaka mitatu iliyopita Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana amezunguka kila kona ya nchi akikinadi chama chake, hii ni aina ya
kampeni ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Kwa upande wa upinzani hali iko
tofauti. Mgombea wao, Lowassa alikuwa mwanachama wa CCM miezi miwili iliyopita,
kuingia kwake Chadema kumeleta mpasuko huku Katibu Mkuu wake akitokomea
kusikojulikana, na Mwenyekiti wa CUF, Lipumba naye akijiuzulu uongozi kupinga
Lowassa kukaribishwa Ukawa. Hii inaonyesha hali si shwari katika upinzani. Kwa
sasa Ukawa wanaficha mpasuko huo kwa propaganda lakini madhara yatajitokeza
kabla ya siku ya uchaguzi. Moja ya viashiria vya mpasuko katika Ukawa ni
kuvunjika kwa makubaliano ya kuweka mgombea mmoja wa Ubunge katika kila jimbo.
Zaidi ya asilimia 70 ya majimbo yana wagombea Ubunge toka vyama vyote
vinavyounda Ukawa. Kwa mfano Lowassa, kama mgombea Urais wa Ukawa, akienda
Ubungo ambapo kuna wagombea toka Chadema, CUF na NCCR atamnadi mgombea yupi?
8. Kuondoka kwa Dr Slaa Chadema,
tuhuma za Mbowe kuiuza Chadema kwa Lowassa kwa TZS bilioni 10 (ambazo Dr Slaa
amezithibitisha) na ukawa kuhama kutoka kumuita Edward Lowassa fisadi mkuu wa
nchi miaka michache iliyopita hadi sasa kumfanya kuwa mgombea wao. Hii
imewakanganya Watanzania wengi na wote wanaochukua muda kulitafakari wanazidi
kupata maswali zaidi. Uamuzi wa mpigakura katika hali kama hii ni kuendelea
kulipigia kura zimwi alijualo (CCM) kuliko zimwi jipya asiloelewa (Ukawa).
9. Matumizi makubwa ya fedha katika
kutafuta madaraka. Mpaka mwisho wa mwezi Agosti 2015 Lowassa alikuwa tayari
ametumia zaidi ya TZS bilioni 106 kwa kipindi cha miaka miwili na nusu kwanza
kutafuta nafasi kugombea ndani ya CCM na kisha kuhamia Ukawa. Wananchi wengi
wanahoji zinapotoka fedha hizi, wengi wakikumbuka kauli ya Mwalimu Nyerere
kwamba “Mtanzania wa leo hawezi kukununua kabla ya yeye kwanza kununuliwa”.
Wananchi wanahoji namna gani Lowassa anapanga kurejesha fedha hizi iwe zake
(pia wanahoji kazipataje) au za marafiki zake (lengo lao kumpa fedha ni nini).
Magufuli hana kashfa ya namna hii na hata kampeni zake za kuomba kuteuliwa
ndani ya CCM hazikuwa za matumizi ya fedha kabisa. Kama wananchi watapiga kura
kwa kuangalia uadilifu katika kupata na kutumia fedha, na pia kama watapiga
kura wakiamini kwamba Ikulu si mahali pa kufanya biashara ili mtu arejeshe
fedha alizotumia wakati wa kampeni na kuhonga kupata nafasi basi Magufuli ana
nafasi kubwa ya kushinda.
10. Mzimu wa Mwalimu Nyerere: Mwaka
1995 Mwalimu Nyerere alisema wazi kwamba Lowassa hafai kuwa Rais wa Tanzania,
alikatwa jina lake kwa haki (video ya Mwalimu akisema haya iko mitandaoni na ni
moja ya video zinazotazamwa kwa wingi wakati huu wa uchaguzi mkuu) na hakuna
maana kuendelea kumjadili na kwamba chama kisonge mbele. Watu wanaomjua vizuri
Lowassa na shughuli anazozifanya wanasema kwa miaka 20 Lowassa hajabadili zile
sifa zilizomfanya Mwalimu kutamka maneno yale mwaka 1995. Hata alipoomba
familia ya Mwalimu Nyerere kumuunga mkono alipoondoka CCM alijibiwa wazi kwamba
yeye hajawahi kuwa chaguo la Mwalimu. Watanzania bado wanamuheshimu na
kumuamini Mwalimu Nyerere na ni wazi watachagua kiongozi wakifuata wosia wake.
Uadilifu wa Magufuli utamuwezesha kuaminiwa na Watanzania na kushinda nafasi
hii.
chanzo:uchaguzi mkuu
0 comments: